6 wapandishwa kizimbani akiwemo mtuhumiwa wa meno ya tembo - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Wednesday, November 16

6 wapandishwa kizimbani akiwemo mtuhumiwa wa meno ya tembo

 Na Mustafa Ismail
Watuhumiwa sita wamepandishwa kizimbani kwenye mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es salaam  kwa makosa ya kuhujumu uchumi, miongoni mwao akiwemo mtuhumiwa wa meno ya tembo Yusuf Ali Yusuf almaarufu mpemba.
Katika kesi hiyo ya Uhujumu uchumi namba 53 ya mwaka 2016, Mshatikiwa namba moja Bw Yusufu Ali Yusufu maarufu kama Mpemba, Charles Mahungo Mrutu, Benedictus Vintus Kungwa, Jumanne Ramadhan Chima, Ahmed Ambari Nyagongo na Pius Vicent Kulangwa wanashitakiwa na kosa la kwanza, ambapo mnamo Januari 2014 na Oktoba 2016 kwenye maeneo ya Dar es salaam, morogoro, iringa, Tanga na Mtwara kwa pamoja na mtuhumiwa mwingine ambaye hajafikishwa mahakamani, inadaiwa walikutwa na meno ya tembo vipande 50 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milion 392.8 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Shtaka la Pili linalowakabili watuhumiwa hao ni kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa oktoba 26 mwaka 2016 katika eneo la mbagala Zakheim wilayani Temeke jijini Dar es salaam walikutwa na Vipande vya meno ya Tembo kumi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milion 65.46 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Shtaka la tatu la watuhumiwa hao ni kumiliki nyara za serikali kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa Oktoba 27 mwaka 2016 katika eneo la tabata Kisukulu Wilayani Ilala jijini Dar es salaam walikutwa na vipande vinne vya meno ya Tembo kinyume na sheria vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milion 32.73 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Shtaka la Nne kwa watuhumiwa hao ni kumiliki Nyara za Serikali kinyume cha Sheria, ambapo inadaiwa oktoba 29 2016 katika eneo la Tabata Kisukulu wilayani Ilala jijini Dar es salaam watuhumiwa walikutwa na meno ya Tembo vipande 36 vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milion 294.61 bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi wa Wanyama Pori.

Katika Kesi hiyo inayosikilizwa na hakim Mfawidhi wa mahakama ya hakim mkazi kisutu jijini Dar es salaam Bw Thomas Simba, Wakili wa Serikali Bw Paul Kadushi, amesema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba kesi hiyo itasikilizwa kwenye Mahakama ya Rushwa na uhujumu Uchumi.

Washitakiwa hao ambao hawakutakiwa kujibu lolote kuhusiana na kesi hiyo, waliiomba mahakama kuwapatia kibali cha kwenda kupatiwa matibabu kutokana na kile walichoelezwa kupata majeraha na maumivu kutokana na kipigo walipokipata walipokamatwa, ombi ambalo Hakim Thomas Simba aliwaagiza watuhumiwa hao kwenda kutibiwa kwenye zahanati za Magereza.
Kesi hiyo imehairishwa hadi disemba mosi mwaka 2016 na watuhumiwa wamepelekwa mahabusu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here