KENYA:MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI WAFULA CHEBUKATI ATISHIA KUJIUZULU MASHARTI YASIPOTIMIZWA - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Thursday, October 19

KENYA:MWENYEKITI WA TUME YA UCHAGUZI WAFULA CHEBUKATI ATISHIA KUJIUZULU MASHARTI YASIPOTIMIZWA

CHEBUKATI ATISHIA KUJIUZULU MASHARTI YASIPOTIMIZWA

Wafula Chebukati
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati.

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati Jumatano alitoa masharti makali, akitishia kujiuzulu yasipotimizwa ili kumwezesha kuendesha uchaguzi uhuru na wa haki Oktoba 26.
Miongoni mwa masharti hayo ni kwa Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa muungano wa NASA, Raila Odinga, kushauriana ili kusuluhisha mgogoro wa kisiasa unaokumba nchini.
Bw Chebukati pia amewataka maafisa wote wa tume hiyo wanaoshukiwa kuvuruga uchaguzi wa Agosti 8, wajiuzulu mara moja ndipo aweze kuendesha uchaguzi huru na wa haki.

“Nimejaribu kufanya mabadiliko muhimu katika tume lakini yamepingwa na makamishna wengi. Katika hali hiyo, ni vigumu kuwahakikishia Wakenya uchaguzi huru na wa haki.
Ninawaagiza maafisa ambao wametajwa kutowajibikia majukumu yao wajiuzulu ili kutoa nafasi kwa kundi maalumu nililobuni kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa kwa vyovyote vile,” akasema.
Baadhi ya maafisa hao ni Afisa Mkuu Mtendaji Ezra Chiloba, Immaculate Kasait (Mkurugenzi wa Usajili wa Wapigakura), Prof Abdi Yakub Guliye (Kamishna na Msimamizi wa Teknolojia (ICT), Bi Betty Nyabuto (Naibu Afisa Mkurugenzi Mkuu) na James Muhati (Mkurugenzi wa ICT). Bi Praxidis Tororei, ambaye alikuwa Mkuu wa Masuala ya Sheria, alijiuzulu.
Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) ameagiza baadhi ya maafisa hao wachunguzwe kwa kuingilia uchaguzi wa urais wa Agosti 8.
Bw Chebukati alitoa tishio hilo saa chache baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Kamishna wa IEBC, Dkt Roselyn Akombe.
Alielezea masikitiko yake kwa tume hiyo kumpoteza Bi Akombe akisema alikuwa mmoja wa maafisa wake wenye busara ya hali ya juu.
Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, Bw Chebukati alikiri kuwa amekuwa akikabiliwa na wakati mgumu katika juhudi za kumaliza mgawanyiko katika IEBC, hali ambayo imeathiri utendakazi wake.
Kujiuzulu
“Kama wakili, siwezi kuendelea kushurutishwa kukubali maagizo ambayo mimi binfasi ninayapinga. Afadhali nijiuzulu ili kudumisha heshima niliyojenga kwa taaluma yangu kwa miaka mingi. Sitakubali kuhusishwa na vitendo ambavyo vitapelekea kuporomoka kwa msingi wa taifa hili,” akasema.
Akaongeza: “Vitendo vyangu kwa sasa vitalinda hadhi yangu na jina la familia yangu. Siko tayari kutoa kafara hadhi ya jina langu kwa manufaa ya muda mfupi ambayo yatanihukumu milele.”
Alisema tayari anaumwa sana kuwa mwenyekiti ambaye alisimamia uchaguzi ambao matokeo yake yalitupiliwa mbali na Mahakama ya Juu.
“Siwezi kuendelea kuongoza tume ambayo imegawanyika. Siwezi kusimamia tume ambayo itatumbikiza taifa hili katika machafuko mabaya zaidi ya kisiasa kuliko yale ya 2007/8,”akaongeza.
Alisema hayuko tayari kusimamia uchaguzi wa Oktoba 26 kama Rais Kenyatta na Bw Odinga hawatafanya mashauriano ya uamimnifu ili kumaliza taharuki ya kisiasa nchini.
Suluhu
“Kukutana kwa wawili hao kutaandaa mazingira yafaayo kwa utendakazi wa tume na wafanyakazi wake wote. Uchaguzi mzuri hauwezi kufanywa katika mazingira ya sasa,” akasema. Alitoa wito kwa viongozi wa kidini, mashirika ya kijamii na jamii ya kimataifa waisaidie nchi kusuluhisha mgogoro uliopo wa kisiasa.
“Ninakubali kuwa tunachohitaji nchini ni Mjadala wa Kitaifa. Kwa sababu hiyo, ninatoa wito kwa wadau wote wakuu wa kisiasa waeleleze juhudi zao za kuandaa mjadala huo ili kuiokoa nchi yetu,” akasema.
Bw Chebukati pia alielezea wasiwasi wake kuhusu kujiondoa kwa Bw Odinga katika uchaguzi akitaja hatua hiyo kuwa “suala nzito.”
“Ni lazima tufikirie athari za kujiondoa kwake na wapigakura zaidi ya milioni sita waliompigia kura. Hatuwezi kuendelea tu kama kwamba kujiondoa kwake hakuna maana yoyote,” akaeleza.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here