Polisi yaua watatu Kibiti - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Thursday, October 19

Polisi yaua watatu Kibiti



KAMANDA WA KANDA MAALUM, LAZARO MAMBOSASA.

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaua kwa kuwapiga risasi watuhumiwa watatu wa ujambazi, lilipokuwa katika doria ya kuwasaka watu wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya Kibiti mkoani Pwani.

Polisi wamesema baada ya kuwapekuwa, watuhumiwa hao walikutwa na mabomu saba, SMG moja ikiwa imefutwa namba zake na ‘magazine’ moja ndani yake ikiwa na risasi 16, maganda 10 ya SMG na pikipiki aina ya Fekon.

Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliwaambia waandishi wa habari jijini jana kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa Jumatatu maeneo ya Msongola wilayani Ilala.

Mambosasa alisema askari wake wakiwa katika doria ya kusaka watuhumiwa wa mauaji ya Kibiti, walitilia shaka pikipiki iliyokuwa imebeba watu watatu ikiwa haina namba.

“Polisi walianza kuifuatilia na walipogundua kuwa wanafuatiliwa waliongeza mwendo na kukatisha njia kuingia barabara ya vumbi na walianza kufyatua risasi na polisi walijibu mashambulizi na kuwajeruhi,” alisema.

Kamanda Mambosasa alisema baada ya watuhumiwa hao kupigwa risasi walianguka na pikipiki yao.

“Katika upekuzi, watu hao walikutwa na silaha aina ya SMG moja ikiwa imefutwa namba zake na magazine moja ikiwa na risasi 16, maganda 10 ya SMG, mabomu aina ya Graned saba na pikipiki moja aina ya Fekon,” alisema Kamanda Mambosasa.

Aliongeza kuwa watu hao ambao wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 40 hawakutambuliwa majina yao na juhudi za kuusaka mtandao waliokuwa wakishirikiana nao zinaendelea.

Alisema watuhumiwa hao walipofikishwa Hospitali ya Temeke, daktari wa zamu siku hiyo alithibitisha walikuwa wameshafariki dunia na miili yao imehifadhiwa hospitalini hapo.

Katika tukio lingine, Kamanda Mambosasa alisema wamewaua watuhumiwa wengine wawili wa ujambazi eneo la Kibonde Maji, Mbagala Zakheim jijini Dar es Salaam.

Alisema watuhumiwa hao waliuawa Jumamosi usiku wakati askari wakiwa katika doria na kupata taarifa kuwa kuna majambazi wamepanga kupora katika maduka ya M-Pesa na Tigo-Pesa.

“Polisi walifika mapema na kuweka mtego wao ndipo ilipofika saa mbili usiku watuhumiwa walikuja na pikipiki moja ikiwa haina namba wakiwa wamebebana watatu,” alisema.

Kamanda Mambosasa aliongeza kuwa wawili kati yao walishuka na kumuacha mmoja kwenye pikipiki ambaye alidai ndiye aliyekuwa dereva wao.

Alisema askari walipowafuata ili wawakamate, dereva wa pikipiki alishtuka na kukimbia na mmoja wa majambazi alichomoa bastola na kufyatua risasi ndipo polisi walipojibu mapigo.

Alisema polisi waliwashambulia kwa risasi na kuwajeruhi watuhumiwa wawili ambao baada ya upekuzi walikutwa na bastola ikiwa na magazine yake na risasi moja na maganda matano ya risasi.

Alisema silaha hiyo ilikuwa imepakwa rangi nyeusi ili kuficha utambuzi wa aina ya silaha hiyo, lakini uchunguzi umebaini kuwa ni bastola aina ya CZ ambayo imefutwa namba zake.

Alisema watu hao walifariki dunia na miili yao imehifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ikisubiri kutambuliwa.

Kamanda Mambosasa pia alisema wanawashikilia watu tisa akiwamo raia wa Yemen ambao wanadaiwa kujihusisha na vitendo mbalimbali vya uhalifu.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa maeneo ya Magomeni Mikumi baada ya kupokea taarifa ya kuwapo kwa mtandao huo.

Alisema watuhumiwa hao walikutwa na magari mawili wanayodaiwa kuwa ni ya wizi, mirungi bunda sita, simu 100, kompyuta mpakato tatu huku mmoja wao akibainika ni mhamiaji haramu.

Kamanda Mambosasa alisema watuhumiwa hao walikutwa na magari mawili yanayohisiwa kuwa ni ya wizi na ndani ya magari hayo kulikutwa na namba za bandia ambazo ni T 937 DJE aina Toyota IST rangi ya bluu bahari na T 774 DHY ambazo gari lake halikufahamika.

Alisema ndani ya gari hilo kulikutwa simu 100, kompyuta mpakato tatu na nyaya mbalimbali na kwamba gari jingine lilikutwa na namba za bandia ambazo ni T 375 CQP aina ya Toyota Vits rangi ya fedha.

Kamanda Mambosasa alisema katika mahojiano na watuhumiwa hao, ilibainika mmoja wao aitwaye Osman Ahmed (25) ni raia wa Yemen ambaye anaishi nchini bila kibali.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here