MALI ZA VIGOGO 500 KUBANWA - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Tuesday, December 6

MALI ZA VIGOGO 500 KUBANWA

Na Mustafa Ismail
Serikali imesema itafanya uhakiki wa mali za viongozi wa umma takribani 500 nchini ili kuthibitisha uhalali wa mali zao.

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angella Kairuki katika uzinduzi wa wiki ya kutoa huduma kwa wananchi katika kuadhimisha Siku ya Maadili kitaifa na haki za binadamu.
Kairuki alisema wamedhamiria kufanya uhakiki huo ili kuhakikisha uhalali wa mali za viongozi wa umma na kupata picha halisi ya mali walizoziorodhesha, lengo likiwa ni kukemea viongozi wanaotoa matamko katika Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo sio ya kweli huku wengine wakificha mali zao.
“Tumekuwa tukifanya uhakiki kwa baadhi ya viongozi, lakini mwaka huu tumedhamiria kufanya uhakiki kwa mali za viongozi wa umma 500, naamini tutapata uhalali na kukemea viongozi wanaotoa matamko ambayo sio ya kweli na wengine wakificha mali,” alieleza Kairuki.
Viongozi wanaowajibika kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma wapo 15,624 ambao wanapaswa kujaza tamko la mali zao kila mwaka na kuliwasilisha kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Kumekuwa na kilio cha muda mrefu katika jamii, kwamba viongozi wengi wamekuwa wakidanganya katika tamko la mali zao kwenye sekretarieti hiyo na hivyo kutaka kuwapo kwa uwazi zaidi katika kusimamia suala hilo, hasa kwa kuwa hakuna urahisi wa mtu kufuatilia fomu hizo na kupinga kile kilichojazwa.
Aidha, waziri huyo alisema ili kupambana na masuala ya rushwa, serikali ina lengo la kuifanyia marekebisho Sheria ya Rushwa ya Mwaka 2007 ili kuweka adhabu kali ambayo itahakikisha kwamba yeyote ambaye atafanya kosa la rushwa afidie hasara aliyoisababisha pamoja na adhabu nyingine ya vifungo jela.
“Adhabu inayotolewa kwa sasa ni ndogo ukilinganisha na kosa analolifanya tutafanyia kazi lengo letu kubwa kwa mwaka huu kuhakikisha kwamba kweli tunakuwa na mapambano ya ufisadi,” aliongeza waziri huyo mwenye dhamana ya kuangalia masuala ya utawala bora.
Aliongeza kuwa serikali haitosita kuifanyia marekebisho sheria yoyote ili kuipa nguvu katika taasisi za uwajibikaji na tayari wameifanyia marekebisho Sheria ya Manunuzi ya Umma na imetoa nguvu kubwa kwani imeangalia maeneo mengi na kuhakikisha thamani ya fedha katika manunuzi inakuwepo.
“Haiwezekani katika halmashauri unakuta manunuzi kama bati linanunuliwa shilingi elfu ishirini na saba hadi thelathini, lakini katika soko unaweza kulipata kwa shilingi elfu kumi na mbili hadi shilingi elfu kumi na nne; hatukubaliani nalo lazima tutunge sheria kali za kuwabana,” alieleza Waziri Kairuki.
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kupambana na rushwa na ufisadi, ukiukwaji wa maadili na kutowajibika kwa watumishi na viongozi wa umma.
Aidha, Dk Mwakyembe alisema serikali itaendelea na mapambano dhidi ya ubadhirifu, wizi na ufujaji wa mali na fedha za umma na yote hayo yatafanikiwa ikiwa kila kiongozi atatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia maadili, sheria na kuheshimu haki za binadamu.
“Ikumbukwe kwamba ubadhirifu, wizi, rushwa na ufisadi umechangia katika kudumaza ukuaji wa uchumi wa nchi yetu na hivyo kuendeleza hali ya umaskini wa wananchi walio wengi ,wakati wachache wakineemeka,” alisema Dk Mwakyembe.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola aliwataka wananchi wanapotilia shaka miradi ya kijamii inayotekelezwa na halmashauri, watoe taarifa katika ofisi zao zilizopo katika kila wilaya.
Kamishna Mlowola alisema wameamua kuunda madawati ya ufuatiliaji kila halmashauri kwa kuwa fedha nyingi za serikali zinakwenda kwenye miradi ya halmashauri.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here