AZAM FC itakutana na Simba SC katika fainali ya Ligi Kuu ya
Vijana chini ya umri wa miaka 20 baada ya usiku wa jana kuitoa Mtibwa Sugar ya
Morogoro kwa penalti 4-2 katika mchezo wa Nusu fainali, kufuatia sare ya bila
kufungana ndani ya dakika 120.
Matokeo hayo yanaifanya Azam FC U-20, kukata tiketi ya
kuchuana na Simba kwenye mchezo wa fainali kesho Jumapili, utakaofanyika Uwanja
wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam saa 1.00 usiku.
Kama ilivyokuwa kwa Azam FC U-20, Simba nayo ililazimika
kusubiri hadi changamoto ya kupigiana mikwaju ya penalti ili kuitoa Stand
United, kufuatia muda wa kawaida wa mchezo na dakika 30 za nyongeza kuisha kwa
sare ya bao 1-1 na hivyo wekundu hao kushinda 8-7.
Washmabuliaji wa Azam FC U-20, Shaaban Idd na Sadalah
Mohamed, itabidi wajilaumu wenyewe baada ya kushindwa kumaliza mchezo huo
mapema kutokana na kukosa umakini kila walipolikaribia lango la wapinzani wao
na kujikuta wakipoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao.
Mchezo huo kwa kiasi kikubwa ulikuwa na ushindani mkubwa kwa
pande zote mbili, ambazo zilikuwa zikicheza kwa kasi kila zikipata mpira hali
ambayo iliwafanya mabeki wa timu hizo kufanya kazi kubwa ya kuokoa hatari zote.
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgsAArqCgO9-oklyJznV48bltSxwvNm32qpMpadNEI7lZLGgj0qmV19ImWWkTdTmDqNC2dg1lmiQ9-Z5kg3Jyn-Ul1QAgROotpYlvlkJ1BtmLOTVyNdQ65HKVlP25TqHJY_rMfXx3hLUcE/s640/IMG_2349+%25281%2529.jpg)
Safu ya ulinzi ya Azam FC U-20, iliyokuwa chini ya kipa
anayeibukia kwa kasi Metacha Mnata, mabeki Abbas Kapombe, aliyekuwa nahodha wa
mchezo huo, Joshua Thawe, Godfrey Elias na Ramadhan Mohamed, ilifanya kazi
nzuri usiku huo wakihakikisha wachezaji wa Mtibwa hawaleti madhara langoni
mwao.
Wachezaji wa Azam FC U-20 walipata penalti zote nne
walizopiga kupitia kwa Rajab Odasi, Joshua, Adolf Bitegeko na Shaaban,
aliyefunga penalti ya ushindi huku Mtibwa itakayocheza na Stand United kuwania
nafasi ya tatu kesho saa 10.00 jioni ikipata mbili tu na kukosa idadi kama hiyo
hiyo.
Vijana hao wa Azam FC, waliingia kwenye mchezo huo wakiwa na
mapengo kadhaa ya kuwakosa wachezaji wake tegemeo katika eneo la kiungo,
nahodha Abdallah Masoud ‘Cabaye’, Prosper Joseph, mabeki Mohamed Omary, Said
Issa, waliokuwa na kadi mbili za njano na kufanya benchini iwe na upungufu wa
wachezaji wanne na kuwa na wachezaji watatu wa kubadilisha akiwemo kipa.
Kikosi cha Azam FC U-20 jana: Metacha Mnata, Salum Isihaka/Omary Wayne,
Ramadhan Mohamed, Abbas Kapombe, Joshua Thawe, Adolf Bitegeko, Godfrey Elias,
Stanslaus Ladislaus/Charles Ndahaze dk 75, Shaaban Idd, Sadalah Mohamed, Rajab
Odasi
No comments:
Post a Comment