Ni umafia kama filamu mauaji ya ‘Msauzi’ Dar - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Sunday, August 20

Ni umafia kama filamu mauaji ya ‘Msauzi’ Dar


WAYNE LOTTER (52).

KIFO cha mwanaharakati kinara wa kupambana na ujangili wa tembo, raia wa Afrika Kusini (maarufu Sauzi), Wayne Lotter (52) , ni kama filamu zile za unyama wa kimafia kwa namna kilivyotokea jijini Dar es Salaam juzi, eneo la Masaki.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo zilithibitishwa na Polisi, ni kwamba wauaji wa Lotter walionekana kumfuatilia muda mrefu kwa mbinu za kihalifu za hali ya juu, wakamuwekea mtego kisha wakafanikisha mauaji yake kwa kumpiga risasi kadhaa mwilini ambazo mwishowe ndizo zilizomsababishia umauti.

Aidha, inaelezwa kuwa mtu aliyejifunika uso kwa namna ileile wanayoonekana kufanya maninja wa kwenye filamu za kibabe, ndiye aliyefanikisha unyama huo baada ya kumuwekea kizuizi marehemu Lotter, majira ya saa tano usiku, wakati akiwa barabarani katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam.

Lotter ni Mkurugenzi wa PAMs Conservation Foundation , asasi maarufu duniani kwa mapambano dhidi ya ujangili hasa wa tembo na tayari, baadhi ya vyombo vya habari vya nje vimekuwa vikihusishwa kifo chake na msimamo wake dhidi ya majangili .

Akielezea tukio hilo jana, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lucas Mkondya, alisema kuwa Lotter aliuawa wakati akiwa kwenye teksi yenye namba za usajili T 499 DEV, aina ya Toyota Sienta.

Kamanda Mkondya alisema katika gari hilo, Lotter alikuwa na mfanyakazi mwenzake aitwaye Christine Clarkl, ambaye pia ni raia wa Afrika Kusini na walikuwa wakitoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, wakitokea Arusha.

Alisema walikumbana na tukio hilo wakati wakiwa njiani kuelekea kwenye nyumba za kupanga zilizopo eneo la Masaki kwa ajili ya mapumziko na ndipo gari moja lisilojulikana lilipotokea na kuwazuia kwa mbele.

Alisema tukio hilo lilitokea katika makutano ya barabara ya Haile Selassie na Kaole Masaki.

“Mtu huyu (muuaji) alikuwa amevaa koti jeusi na kufyatua risasi mbili akidai apewe dola … risasi ilimjeruhi Lotter mdomoni na alifariki wakati akikimbizwa hospitali ya Sami iliyopo Masaki kwa ajili ya kupatiwa matibabu,” alisema Kamanda Mkondya.

Aidha, alisema wahalifu hao walipora kompyuta mpakato tatu aina ya Dell, simu moja aina ya Nokia na nyaraka mbalimbali.

WAZIRI MALIASILI ASHTUSHWA
Kwa upande wake, Waziri wa Mali Asili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, jana alielezea kuguswa kwake na msiba huo na kutoa pole kwa familia na taasisi ya Lotter kwa kupoteza mpendwa wao na kuomba wawe watulivu wakati Jeshi la Polisi likifanya uchunguzi kuhusiana na mauaji hayo.

“Natoa salamu za pole kwa familia yake, kwa marafiki zake na nchi yake kwa sababu alikuwa mshirika wetu katika kupambana na ujangili, hatujui nia wala ni nani ambaye amefanya yale mauaji,” alisema na kuongeza.

“Polisi wanafanyia kazi mauaji hayo na mwelekeo wa polisi wa kuwafikia wauaji uko karibu… naomba tusubiri ili tujue ni kitu gani kilichotokea kwa huyu mtu,” alisema Waziri Maghembe.

Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja kutoka taasisi ya marehemu, Wayne alijitoa maisha yake kulinda na kuhifadhi wanyamapori Afrika, akifanya kazi kama askari wanyamapori aliyeongoza mapambano dhidi ya ujangili Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Wayne alikuwa mtu anayejali watu na maisha ya wanyama na mwaka 2009 alijiunga na timu ya Krissie Clark na Ally Namangaya, iliyoanzisha Pams Foundation.

“Wayne aliamini jamii ndiyo watetezi wa wanyama, miongoni mwa kazi alizofanya ni kutoa mafunzo kwa maelfu ya vijana Tanzania wanaosimamia rasilimali za taifa kama wanyama na misitu,” ilisema taarifa hiyo.

Pia ilieleza kuwa, uchangamfu wake, umahiri wake wa kazi na utu wake vilimfanya kuwa wa kipekee hivyo kuwafanya hata walio karibu naye kuwa wenye furaha muda mwingi.

Wakati huo huo, Waziri Maghembe aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wamekamata meno ya tembo 28 yenye uzito wa kilogramu 366 ambapo meno 21 yamekutwa kwenye ghala na saba nyumbani kwa mtu.

Alisema inaonekana uhalifu huo ulifanyika kati ya mwaka 2013/14 na wahalifu kuyaficha na kuyauza kidogo kidogo.

Aliwataja watuhumiwa kuwa ni pamoja na Bakari Seruni ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mbezi Beach, Juma Yebo, Hamis Omar, Mohamed Yahaya, Hamis Shelukindo na Ahmed Bakari ambao wanashikiliwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here