Simba SC wapitisha mfumo wa kuuza Hisa, Wanachama wapewa asilimia 10 Papo Hapo - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Sunday, August 20

Simba SC wapitisha mfumo wa kuuza Hisa, Wanachama wapewa asilimia 10 Papo Hapo


WANACHAMA 1,216 wa klabu ya Simba, leo wameridhia mfumo wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Salim Abdallah 'Try Again' alisema kwamba asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo.

Abdallah alisema mwekezaji huyo au hao, wanatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.

Alisema asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali, hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.

Na baada ya mkutano wa leo, zoezi litakalofuata ni uhakiki wa wanachama wa klabu hiyo ili kuweza kujua mgawanyo wa asilimia 10 za hisa utakavyokuwa – na itaundwa Kamati maalum ya kupitia maombi ya wawekezaji wanaotaka kununua asilimia 50 ya hisa.

Mgeni rasmi, Dk Kigwangala ameunga mkono mabadiliko hayo na kuwaambia wanachama wa Simba wamechelewa kufanya uamuzi wa mabadiliko hayo, kwani walipaswa kufanya hivyo miaka mingi iliyopita na anaamini klabu nyingine zitafuata nyayo hizo.

“Leo Agosti 20 klabu ya Simba imetengeneza rekodi  nyingine baada ya ile ya mwaka 1977 ya kuwafunga Yanga 6-0, na sisi kama Serikali chini ya rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli tunaunga mkono mabadiliko ya uendeshwaji wa klabu ya Simba,”amesema Dk. Kigwangala.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here