Na Mustafa Ismail
RAIS John Magufuli amezindua ndege mpya mbili za serikali
zilizonunuliwa aina ya Bombardier Dash 8 Q400 huku akiwapasha wale waliokuwa
wakibeza ununuzi wa ndege hizo, akitaka Bodi mpya ya Kampuni ya Ndege Tanzania
(ATCL) kutosita kuwafukuza kazi wafanyakazi watakaobainika kuhujumu kampuni
hiyo.
Aidha, ametangaza kuwa serikali imeanza mazungumzo ya
kununua ndege nyingine mbili mpya, ikiwamo itakayokuwa na uwezo wa kubeba
abiria 240.
Kwa upande wao, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
imependekeza ndege hizo kuitwa ‘Hapa Kazi tu’ iwapo Rais ataridhia jina hilo
kwani serikali haijanunua ndege mpya tangu mwaka 1978. Ndege hizo zitakodishwa
kwa ATCL.
Uzinduzi huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Julius Nyerere (Terminal 1), Dar es Salaam, ulihudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa serikali akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Spika
wa Bunge, Job Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Makatibu
Wakuu na Mawaziri wa wizara mbalimbali.
Rais Magufuli amesema watu wengi wamekuwa wakibeza ununuzi
wa ndege hizo zilizotengenezwa nchini Canada na wakati mwingine alifikiria kwa
nini aliamua kufanya jambo hilo; kwani wengine wamekuwa wakisema haina spidi na
wengine kuwa ni mkweche, jambo ambalo siyo la kweli na kusema watu hao watakuwa
wa kwanza kupanda kwani zinatumika na nchi nyingine kama Marekani wanazo 40 na
pia Ethiopia.
“Wengine walilalamika kwa nini tumenunua kwa fedha taslimu,
sasa mtu ukiwa tajiri kwa nini usinunue ‘cash’, kwa nini ukopeshwe ili watu
wapate faida, kuna fedha za Watanzania na wanataka ndege ndiyo maana tukanunua
‘cash’, ” alisema Rais Magufuli.
Amesema ndege hizo ni nzuri na ukitaka kujenga uchumi wa
kisasa lazima uwe na ndege na ukitaka kuwa na watalii hakuna sababu ya
kuwafanya waende kwenye nchi nyingine ili waje nchini mwenu lazima ziwepo
ndege.
Rais Magufuli amesema kwa ndege ya aina ya Jet kutoka Dar es
Salaam kwenda Songea unatumia mafuta ya Sh milioni 28.5 lakini ukitumia ndege
hizo mpya unatumia Sh milioni moja kwa umbali huo wakati kufika tofauti yake ni
dakika 20 tu.
Amesema wanaopiga vita ni wafanyabiashara, hivyo kama
wanataka spidi wakapande za jeshi ili wafike haraka wanapotaka kwani inafanyika
biashara lazima kuangalia mazingira yote na viwanja vyote kutumika.
Amesema nauli ya kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ni Sh
800,000 lakini hizi hazitafika huko na uzuri wa ndege hizo zitatua katika
viwanja vya ndege vya mazingira yote nchini.
Rais aliwaomba Watanzania kutopuuza vitu vyao na kama hataki
ni kukaa kimya na kuacha kiherehere na kuzoea kusifia wengine na kuhoji, kwa
nini wasisifie vya kwao kwani ndege hiyo itatumika na watu wa itikadi
mbalimbali kwa kuwa ni ya Watanzania.
“Ni lazima Watanzania kujifunza kujivunia vya kwao… lazima
mfahamu kwa kulipa ndege hizo polepole tungelipa gharama kubwa tofauti na
tulivyolipa fedha taslimu, tumepunguza gharama na tuna mpango wa kununua ndege
mbili kubwa na fedha zipo,” alisema.
Ameeleza kuwa ndege hizo ipo itakayokuwa na uwezo wa kubeba
watu 160 na nyingine 240 na kwamba yalipofanyika majadiliano wahusika walikuwa
wanaweka muda mrefu kwa kusema ndege ya abiria 240 italetwa mwaka 2021, lakini
tunajadiliana ili kuzipata mapema na fedha zipo.
Amesema ndege hizo zikinunuliwa itaondoka Dar es Salaam
mpaka Marekani, China bila kutua na itawawezesha watalii kutoka nchini mwao na
kuingia moja kwa moja hapa nchini bila kupitia nchi nyingine. Alitaka wizara
kuendelea na mchakato kwa kuitisha kampuni ili uwepo ushindani na kununua kwa
bei nafuu kwani wananunua kwa fedha taslimu.
Amesema ndege hizo mbili mpya zilizozinduliwa jana
wanazikodisha kwa ATCL na kuwataka kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwa
kutengeneza bodi nzuri ya wasomi wakati Mkurugenzi Mkuu wa ATCL akitokea nchini
Senegal alipokuwa akifanya kazi huko hivyo mwendo wa kucheza umekwisha.
Alielezea baadhi ya vitu vilivyofanya ATCL kutofanikiwa kuwa
ni pamoja na kutokuwa na mfumo
wa kujiendesha kwa kujitegemea kibiashara muda
wote kutegemea serikali, kubweteka kwa wafanyakazi wake, hujuma ya wafanyakazi,
kutengeneza hasara za ajabu ajabu, mafuta hewa kwa kudanganya ndege imesafiri,
lakini kumbe bado iko hapo hapo pamoja na kujilipa malipo ya ziada.
Amewaomba bodi na wizara kutokuwa na huruma kwa wasiofaa kwa
kuwafukuza kazi kwa
kuchambua kweli kweli na kuwachekecha ili kupata watu wanaotaka
kubadilika na kuwaomba wafanyakazi wanaotaka kufanya kazi kweli kujisalimisha.
“Nakueleza waziri usiogope kupunguza wafanyakazi kama
tulipunguza NIDA 600 hatuwezi kushindwa hawa 200 kwa ambaye hawezi kwenda na
spidi yetu atupishe na kwenda na waliojipanga kwenda kwa spidi tunayotaka
wengine wape fedha zao wapumzike, kwani tunataka siku moja shirika hili liwe na
ndege hata 10,” alisema.
Ameomba uongozi wa ATCL kutotumia mawakala kukatisha tiketi
ila wazingatie huduma watakazotoa na huku akikosoa sare za wafanyakazi ambazo
alisema zinatia kichefuchefu na kuwataka kujipanga vizuri ili walipakodi waone
matunda yake.
Ameomba pia bodi na menejimenti kutoruhusu kiongozi wa
serikali kusafiri bure hata kama ni yeye au waziri wa wizara hiyo au bodi kwani
kuna wakati wanakuwa wanajipendekeza wakati wanatakiwa kufanya biashara.
Akizungumzia uboreshaji wa Reli ya Kati, Rais Magufuli
alisema kwa sasa ujenzi wa reli mpaka Mwanza na Isaka mpaka Burundi zabuni
zimetangazwa na fedha zipo.
Amesema kwa reli ya zamani umepatikana mkopo kutoka Benki ya
Dunia na mabehewa yameongezeka na siku zijazo Dar es Salaam itakuwa na treni ya
umeme kwani haya yanawezekana siyo Ulaya tu hata hapa nchini yatafanyika.
Akizungumzia ununuzi wa ndege hizo, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema mara ya mwisho kwa
serikali kununua ndege mpya ilikuwa 1978 na shirika lilikuwa likitumia ndege za
kukodisha na kusababisha madeni.
Akizungumzia sifa za ndege hizo mpya, alisema ni miongoni
mwa ndege za kizazi kijacho na kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kutumia
mafuta kidogo huku zikitua viwanja vyote nchini vya lami na visivyokuwa na
lami.
Amesema ndege hizo kila moja ina uwezo wa kubeba mizigo tani
1.6 na abiria 76 na kati yao sita wanabebwa katika daraja la kibiashara na
katika hatua za awali wamejipanga kutoa huduma katika viwanja 12.
Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni Dar es Salaam, Zanzibar,
Mwanza, Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Bukoba, Kigoma, Tabora, Mbeya, Mtwara na
Comoro huku wakiendelea na upembuzi yakinifu ili kuongeza viwanja vingine ili
ndege ziweze kutua.
Amempongeza Rais kwa uamuzi wa kununua ndege hizo na
kuonesha kuwa ni kiongozi wa vitendo kuliko maneno na wanapendekeza ndege hizo
kama rais ataridhia ziitwe ‘Hapa Kazi Tu’.
Naye Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi alisema uamuzi
wa kununua ndege za aina hiyo ulifanyika kwa kuzingatia sifa za kutua na kuruka
katika viwanja vya lami na visivyo na lami, kutumia mafuta kidogo kwenda umbali
mrefu hivyo gharama za uendeshaji kuwa ndogo.
Amesema ndege hizo zina uwezo wa kubeba mzigo mkubwa na
injini zenye kazi hivyo kuimarisha mtandao wa usafiri wa anga na unafuu wa bei
na kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji.
Balozi Kijazi alisema ndege hizo ni za serikali na siyo za
ATCL hivyo wataingia mkataba kwa kukodisha ndege kwa kampuni hiyo na kuzilipia
hivyo lazima kampuni hiyo kujipanga kuingia katika ushindani wa usafiri huo.
SOURCE:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment