Na Mustafa Ismail
RAIS John Magufuli amepokea zaidi ya Sh bilioni sita kutoka
kwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May, kwa ajili ya kusaidia waathirika wa
tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ndege mbili za Serikali,
Rais Magufuli alisema alikabidhiwa fedha hizo jana asubuhi na Balozi wa
Uingereza nchini, Sarah Cooke.
Aidha, Rais Magufuli alisema wadau mbalimbali wametoa fedha
kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko hilo, lakini Katibu Tawala wa Mkoa
(RAS), Amantius Msole pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba,
Steven Makonda, waliamua kufungua akaunti inayofanana na iliyofunguliwa rasmi
kwa ajili ya kukusanya fedha za msaada kwa ajili ya waathirika wa tetemeko na
kuanza kuzitafuna.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, Katibu Tawala huyo pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba walikamatwa jana na kufikishwa
mahakamani mjini Bukoba.
Kutokana na maelezo ya Rais, baada ya Serikali kuchukua
hatua hiyo iliyowapa imani wadau mbalimbali wanaojitolea kuchangia
walioathirika na tetemeko hilo, Ubalozi wa Uingereza ulichanga pauni milioni
2.3 zilizotolewa na Waziri Mkuu wa nchi hiyo.
Rais Magufuli alieleza kuwa Uingereza na wadau wengine
wamekuwa na imani zaidi kuwa fedha wanazotoa zinawafikia walengwa.
Juzi, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Katibu Tawala huyo
wa Mkoa wa Kagera pamoja na Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Halmashauri ya
Manispaa hiyo ya Bukoba, baada ya viongozi hao kubainika kuwa walifungua
akaunti nyingine inayofanana na ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Maafa ya Kagera kwa
ajili ya kujipatia fedha.
Viongozi hao wanadaiwa kufungua akaunti yenye jina “Kamati
Maafa Kagera” linalofanana na la akaunti rasmi kwa lengo la kujipatia fedha kwa
maslahi yao.
Aidha Rais amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk
Charles Kimei awachukulie hatua watumishi wa benki hiyo walioshirikiana na
watumishi hao kufanya njama za kuanzisha akaunti nyingine ya benki yenye jina
linalofanana na akaunti rasmi ya “Kamati ya Maafa Kagera” kwa lengo la
kujipatia fedha.”
SOURCE:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment