TAZAMA MAKONGAMANO YA KIMATAIFA YALIYOILETEA TIJA NCHI YA KENYA 2016 - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Thursday, December 29

TAZAMA MAKONGAMANO YA KIMATAIFA YALIYOILETEA TIJA NCHI YA KENYA 2016

Na Mustafa IsmailMWAKA 2016 ulikuwa wa aina yake katika sekta ya biashara nchini, kwani Kenya ilifanikiwa kuandaa makongamano mawili makubwa ya kibiashara ambayo yaliwakutanisha wadau mbalimbali duniani.

Mawili hayo ni Kongamano la Sita la Tokyo la Kimataifa Kuhusu Maendeleo Barani Afrika (TICAD) na lile la Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Ustawi wa Kibiashara (UNCTAD).
Makongamano haya yalifanyika katika miezi ya Julai na Agosti mtawalia.
Wakati wa makongamano hayo, Kenya ilinufaika kuwili, kwani wafanyabiashara mbalimbali walinufaika sana jijini Nairobi, ikizingatiwa kuwa yalifanyika katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC).
Katika kongamano la TICAD, zaidi ya marais 30 wa nchi mbalimbali barani Afrika walihudhuria, akiwemo Waziri Mkuu wa Japan Bw Shinzo Abe.
Kongamano hilo pia lilichangia pakubwa kuimarika kwa imani ya jamii ya kimataifa kwa Kenya kuhusu hali yake ya usalama, kutokana na msururu wa mashambulio ya kigaidi ambayo imekuwa ikikabiliwa nayo.
Aidha, Afrika ilinufaika pakubwa baada ya Japan kuiahidi msaada wa kifedha wa Sh3 trilioni, ili kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo.
Manufaa
Kenya ilinufaika kwa kupata msaada wa Sh27.3 bilioni za kujenga eneo maalum la kibiashara katika eneo la Dongo Kundu, Mombasa.
Awamu ya kwanza ya mradi huo inatarajiwa kumalizika kufikia mwaka wa 2019. Makubaliano hayo pia yanalenga kuimarisha Bandari ya Mombasa.
Kampuni nne za kimataifa pia zilitoa msaada wa Sh7.6 bilioni kwa mpango wa 'Beyond Zero’ ambao huendeshwa na Mkewe Rais Bi Margaret Kenyatta.
Wawekezaji katika sekta ya kibinafsi nchini pia walipata nafasi ya kuonyesha bidhaa zao mbalimbali.
Kwa pamoja Japan ilitia saini makubaliano ya kibiashara, maarufu kama 'Muafaka wa Nairobi’ ambao unajumuisha kanuni zitakazozingatiwa katika makubaliano hayo, kiasi cha fedha kitakachotolewa kwa nchi husika na miradi ya maendeleo ambayo itafadhiliwa.
Akizungumza baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo, Rais Uhuru Kenyatta alisema kuwa utekelezaji wa mwafaka huo utainua kiwango cha uchumi cha bara Afrika pakubwa.
“Makubaliano yote ambayo yamepitishwa katika kongamano hili yatachangia pakubwa katika ustawishaji wa kiuchumi wa Afrika kwa ujumla,” akasema Rais Kenyatta.
Sekta zitakazonufaika kwenye muafaka huo ni kilimo, ujenzi wa barabara pamoja na ushirikiano wa taasisi za kibinafsi.
Mpango huo wa miaka mitatu pia utachangia pakubwa uimarishaji wa taasisi za afya, ufadhili wa elimu na utoaji mafunzo kwa wahudumu katika sekta ya afya.
Japan pia itashiriki katika mikakati ya kukabiliana na ugaidi, biashara haramu, ufisadi na ushirikiano wa kikanda na kimataifa kuhusu masuala mbalimbali.
Kwenye kongamano la UNCTAD, mawaziri wa biashara kutoka nchi 194 kote duniani walihudhuria.
Ushirikiano
Aidha, kongamano hilo lililenga kupanua ushirikiano wa kibiashara, hasa katika masuala ya uwekezaji na juhudi za kukabiliana na umaskini duniani.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni Bi Amina Mohammed  ndiye aliyeuongoza ujumbe wa Kenya kwenye kongamano hilo, ambapo mkataba wa kibiashara uitwao 'Maafikiano wa Nairobi’ ulitiwa saini na nchi wanachama.
“Ni  hatua nzuri ambayo itapanua ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa mbalimbali kote duniani,” alisema Bi Mohammed.
Maazimio yaliyopitishwa yanatarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka minne ijayo, ambapo kongamano lingine litaandaliwa.
Baadhi ya masuala yaliyozingatiwa katika mkataba huo ni pamoja na upunguzaji wa kodi na ada za forodha katika mipaka, upunguzaji deni miongoni mwa mataifa wanachama, upanuzi wa ushirikiano wa kibiashara kati ya Bara Afrika na kanda nyingine duniani kati ya masuala mengine.
 Kwenye hotuba yake Bi Mohammed alisema kuwa kuandaliwa kwa kongamano hilo nchini ni ishara ya Imani ambayo jamii ya kimataifa inayo kwa Kenya na Afrika kwa jumla.
Katika mkakati wa kupunguza ada za biashara katika maeneo ya mipakani, wanachama hao walikubaliana kuwa nchi husika zishauriane kuhusu njia za pamoja za kutekeleza ada hizo, ili kuhimiza mwingiliano ufaao.
Pendekezo hili lilitolewa na baadhi ya wajumbe kutoka Kenya, wakionekana kurejelea masaibu ya baadhi ya Wakenya ambao wamekuwa wakifanya biashara katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki kama Tanzania na Uganda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here