JPM ACHUKIZWA NA WANAOLETA MZAHA VITA DAWA ZA KULEVYA - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Monday, February 13

JPM ACHUKIZWA NA WANAOLETA MZAHA VITA DAWA ZA KULEVYA

Na Mustafa Ismail
RAIS wa jamuhuri ya muungano wa Tanzania mheshimiwa John pombe Magufuli amesema Watanzania ambao wamefungwa maisha au kunyongwa nje ya nchi baada ya kubainika kuwa wanajihusisha na dawa za kuleya, serikali yake haitajihusisha kwa lolote na watu hao kwani wana haki ya kupewa adhabu hiyo.
Akizungumza Ikulu, Dar es Salaam jana wakati wa kuwaapisha Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya, Rodgers Sianga, Rais Magufuli aliwaagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na mabalozi walioko nje ya nchi, kwamba wasije wakajitokeza kuwaombea msamaha au jambo lolote watu hao ambao wamefungwa kwa makosa ya dawa za kulevya.
“Kama kuna Mtanzania amehukumiwa kunyongwa au kufungwa maisha, waziri na mabalozi wetu mlioko huko msijihusishe kwa lolote, waacheni wapate chakula wanachostahili, hakuna kuwaombea msamaha, waacheni wanyongwe,” alisema Rais Magufuli.
Alisema ameamua kulisema hilo kwa dhati na wala hawezi kumung’unya maneno kwa sababu kama viongozi watachekea jambo hilo, taifa litaendelea kupoteza nguvu kazi nyingi.
Aliwaomba jumuiya za kimataifa kuisaidia Tanzania katika vita hiyo. Rais alisema taarifa alizonazo kuna Watanzania zaidi ya 1,000 ambao wamefungwa nchi za nje na wengine wamehukumiwa kunyongwa.
Wengi wa Watanzania wamekamatwa China ambako kuna Watanzania zaidi ya 290, Afrika Kusini 296 na Brazil ambako kuna Watanzania 120.
Amtetea Makonda, aomba asikatishwe tamaa Rais John Magufuli ametoa ufafanuzi hatua za wakuu wa mikoa kutangaza vita ya kupambana na biashara ya dawa za kulevya kwa kuwa wamepewa mamlaka hayo na Sheria ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2015.
Alisema serikali ni kuanzia Rais, makamu wa rais, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa wilaya.
Alisisitiza wote hao wana jukumu la kupambana na dawa za kulevya kwa kuwa wamepewa mamlaka na sheria hiyo.
Alipongeza Bunge lililopita kwa kutunga sheria hiyo na pia alimpongeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kusaini sheria hiyo.
Alisema serikali itaisimamia sheria hiyo, na hawatajali mtu yeyote, awe mbunge, mwanasiasa, waziri, mchungaji, padri au shehe.
“Tuta deal (shughulika) na mtu yeyote, wale ambao wanadhani sheria hii ambayo inaipa mamlaka Serikali kusimamia vita ya dawa za kulevya haifai, wapeleke bungeni ikafanyiwe marekebisho hasa kifungu cha 10,” alisema Dk Magufuli.
Alisema vita ya dawa za kulevya ni nzito kuliko wanavyotegemea na akaongeza kuwa Tanzania ndio njia ya kupitishia dawa za kulevya, jambo ambalo linahitaji Watanzania wote kushirikiana na sio kubezana au kukatishana tamaa.
Hivyo aliwaomba Watanzania kwamba akitokea mtu ama kiongozi akajitolea kupambana na tatizo hilo, atiwe moyo na sio kubezwa au kumkatisha tamaa kama inavyotokea kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.
Alisema hata kama ni mwanachama wa CCM akikamatwa na dawa za kulevya, chama chake kisihusishwe badala yake mzigo huo auchukue mtuhumiwa mwenyewe. “Kila mtu abebe msalaba wake mwenyewe,” aliongeza.
Akiri PM, mawaziri kufichwa sheria Hata hivyo, alisema sheria hiyo ilikuwa haifahamiki na Waziri Mkuu alifichwa kuhusu sheria hii kwamba yeye ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Kupambana na Dawa za Kulevya.
“Waziri Mkuu mwenyewe amejua jana au juzi kwamba ndiye mwenyekiti wa baraza hilo,” alibainisha Rais Magufuli.
Alisema hana uhakika kama mawaziri husika kwenye baraza hilo walikuwa na taarifa kwamba ni wajumbe kwenye baraza hilo, maana walifichwa na wasaidizi wao wa wizarani hadi pale walipoelezwa na waziri mkuu kwamba wanawajibika katika kupambana na dawa za kulevya.
Alisema kutokana na ugumu uliopo hata ndani ya serikali, ndio maana hakuwahi kupelekewa jina ili ateue kamishna wa mamlaka ya kuzuia na kupambana na dawa za kulevya hadi alipoamua juzi yeye mwenyewe kumteua kwa njia anazozijua yeye.
“Nilikuwa najiuliza kwa nini sijaletewa mapendekezo ya uteuzi wa kamishna wa dawa za kulevya, baada ya kuona kimya nikaamua kuteua mwenyewe, kwa hiyo mnaona vita hii ilivyokuwa kubwa, ndani ya serikali sio malaika,” alieleza.
Aliwataka Watanzania wasishabikie kirahisi mambo hayo, na wengine kuandika hata majina ya bandia kwenye mitandao ya kijamii kama kuharibu majina ya watu.
Alisema vita hiyo ni kama vita nyingine na madhara yake ni makubwa.
Alisema wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni wakubwa ambao hawajali maisha ya watu, bali wanaangalia zaidi kupata faida kubwa na wana uwezo wa kumlipa mtu yeyote kufanikisha malengo yao.
Alisema kupambana na hao watu ni lazima watu wote washiriki na kumtanguliza Mungu.
Amtaka Sianga, PM waache woga Alimwagiza kamishna mkuu wa dawa za kulevya kwamba asiogope, afanye kazi kwa ujasiri ili kuokoa roho za watu hasa vijana.
Hata hivyo alitahadharisha kuwa vita hiyo ni kubwa, aliomba katika vita hiyo wasimwonee mtu yeyote kwa kufanya mizaha mizaha.
Pia alimwagiza waziri mkuu ambaye ndiye mwenyekiti wa baraza hilo kufanya kazi kwa ujasiri na kusimamia sheria hiyo.
Alisema sheria isingekuwa inamtaja waziri mkuu, angejipa yeye jukumu la kuwa mwenyekiti wa baraza hilo, ila hataki kuvunja sheria.
“Usiogope kusimamia hilo kwa kuogopa kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na wewe, wewe hukuzaliwa ukiwa waziri mkuu, mawaziri kasimamieni sheria hii, nashangaa wakati mwingine mawaziri mnakuwa waoga, ni Mungu kawapatia nafasi hizo, fanyeni kazi kwa ujasiri bila kumwogopa mtu,” alisema Rais Magufuli.
Ashangaa mbwembwe Polisi Aidha, Rais Magufuli ameshangazwa hatua ya baadhi ya watu walioitwa na mkuu wa mkoa ambao walienda kuripoti polisi mwishoni mwa wiki kuonesha mbwembwe mbalimbali mbele ya polisi.
“Mtu anapiga deki gari kituo cha polisi, aliambiwa pale polisi ni mahali pa kusafishia gari lake, ninyi polisi mngemweka ndani na hilo gari mngelichukua mkaliweka mahabusu,” alisema na kuongeza, “Eti mtu anakuja na kwaya polisi! Hivi ninyi Polisi mlimwambia mnataka kuimbiwa nyimbo za mapambio?"
“I wish (natamani) ningekuwa IGP...Kamishna Sirro ulitaka kuimbiwa nyimbo za mapambio (Simon Siro akasimama akajibu, hapana mzee), imefikia mahali watu wanakuwa na dharau hata kwenye mambo serious (mambo mazito)... hiyo kwaya ikija siku nyingine kamata wote weka ndani...mbona hawaendi kuimba mapambio yao pale Lugalo". “CDF hivi ungekuwa ni wewe ungekubali kuimbiwa yale mapambio pale jeshini (Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alijibu hapana mzee). Nataka hii hapana CDF iwe hapana kwa majeshi yote, nataka vyombo vya ulinzi viheshimiwe, mmepelekwa pale kusimamia sheria, mkiendekeza mizaha kwa mambo haya tutakuja kujuta,” alisema Rais Magufuli.
Majaliwa aahidi kupambana Naye Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kwamba vita ya dawa za kulevya ni endelevu na hawatamwonea mtu katika mapambano hayo.
Alisema kinachoendelea sasa nchini kote ni mwanzo tu na vita ndio kwanza imeanza.
Alisema kwa kuwa amepatikana kamishna wa mamlaka ya kupambana na dawa za kulevya, anaamini kwamba vita hiyo itanoga vizuri kwani atakuwa ndiye kinara katika mapambano hayo kwa kushirikiana na mamlaka zingine.
Majaliwa alitoa mwito kwa wakuu wa mikoa kuendelea na juhudi za kupambana na dawa za kulevya katika mikoa yao.
Pia alitoa mwito kwa mahakama kuwasaidia ili kesi zilizopo mahakamani zisikilizwe haraka.
Sianga aahidi mazito Akizungumza baada ya kuapishwa, Sianga alisema atapambana na dawa za kulevya kwa kushirikiana na wadau wengine katika vita hiyo.
Alisema atadhibiti uingizwaji, matumizi na pia atajielekeza kuwatibu wale ambao tayari wameathirika.

Alisema kuna watu walitumia dawa za kulevya na wengine kuathirika kwa magonjwa ya HIV, alisema watu hao ni lazima mamlaka yake ishughulike nao ili wasiendelee kuambukiza jamii kubwa.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here