waziri wa kilimo,mifugo na uvuvi Dk Charles Chizeba |
Alisema hayo jana wakati akijibu hoja za wabunge takribani 136 waliochangia katika mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2017/18 iliyowasilishwa bungeni Ijumaa iliyopita.
“Niwaombe wabunge tusipate wasiwasi kwamba kilimo kina bajeti ndogo. Hiki ni moja ya kipaumbele, bila kilimo, viwanda itakuwa ngumu kufanikisha ni kweli kabisa. Israel kipaumbele chao ni usalama, lakini bajeti yao ya ulinzi pamoja na kwamba ni kipaumbele wanapata msaada kutoka Marekani.
Mwaka jana wamepata msaada wa Dola za Marekani bilioni 38 wakati kwenye bajeti ya ndani walitenga Dola za Marekani bilioni 4.6.” Akaongeza, “...Hata sisi wakati tunaweka bajeti tunaangalia wenzetu wanaotuunga mkono wanatupa kiasi gani ili tufanye mgawanyo sahihi wa mahitaji ya ndani.”
Katika michango yao, wabunge wengi walionesha wasiwasi kutokana na bajeti ya wizara hiyo kuendelea kushuka mwaka hadi mwaka huku kiasi cha fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2016/17 kikitolewa kwa asilimia tatu jambo lililowafanya wahoji kuhusu kipaumbele cha serikali dhidi ya kilimo.
Pamoja na hayo pia baadhi ya wabunge walibeza kitendo cha serikali kufuta kodi 108 katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na kusisitiza kuwa kodi zilizofutwa hazimnufaishi mkulima, bali mtu wa kati na mfanyabiashara.
Akihitimisha hoja yake, Waziri Tizeba alisema bajeti ya sekta ya kilimo si yote iliyoko kwenye wizara yake ya Kilimo kwani ipo pia kwenye maeneo ya nje ya wizara hiyo kama vile Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambako huko ndiko kwenye utekelezaji wa shughuli za kilimo na kwenye halmashauri.
“Wizara inajihusisha zaidi na sera na miongozo ya kitaifa, lakini kule kwenye mzizi kunashughulikiwa na Tamisemi. Pia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, nao wanafanyakazi zinazohusu kilimo ingawa si moja kwa moja,” alieleza Dk Tizeba.
Alisema kwa uchache taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo zinakusanya maduhuli na kutumia katika sekta ya kilimo jumla ya Sh bilioni 260 ambapo pia alibainisha kuwepo kwa taasisi nyingi za wabia wa maendeleo wanaochangia kwenye kilimo, lakini si katika mfumo wa serikali.
“Mfano mwaka jana 2015/16, kwa jumla wadau wa maendeleo walichangia shilingi trilioni 1.73 katika kilimo moja kwa moja wakati bajeti ya serikali kwa jumla ilikuwa trilioni 1.01. ukijumlisha ni karibia trilioni 2.7 ni fedha nyingi kuliko wizara nyingine,” alifafanua.
Alieleza kuwa hadi sasa fedha kwenye kilimo ni nyingi katika mwaka huu wa fedha wa 2016/17 kwani hadi bado wafadhili wanaendelea kujitolea fedha katika kilimo ambapo takribani Sh bilioni 400 zimeingizwa kwenye kilimo kupitia miradi mbalimbali.
Akizungumzia tozo zilizofutwa, alisema amesikitishwa kuona kuwa pamoja na jitihada za serikali kuchukua hatua dhidi ya kero zilizokuwa zikiwasumbua wananchi katika tozo na kodi mbalimbali, bado kuna wabunge wanaobeza hatua hiyo.
Alisisitiza kuwa, utitiri wa kodi na tozo zilizofutwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, ulizingatia mnyororo wa thamani na namna zinavyomuathiri mtu mmoja, hivyo maamuzi ya kuziondoa yatanufaisha watu wote.
No comments:
Post a Comment