Cameroon leo watamenyana na Chile kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Otkrytiye Arena mjini Moscow, Urusi, wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia mwakani.
Cameroon na Chile zipo Kundi B pamoja na Australia na Ujerumani, wakati Kundi A lina timu za Urusi, Ureno, Mexico na New Zealand. Urusi ilianza kwa ushindi wa 2-0 jana dhidi ya New Zealand.
Mchezo huo wa Kundi B unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua, Chile ikiongozwa na mshambulaiji wa Arsenal, Alexis Sanchez na Cameroon ikiongozwa na mshambuliaji wa Besiktas ya Uturuki, Vincent Aboubakar.
Kila inapowadia michuano ya Kombe la Mabara, ambayo ilianza jana huja na kumbukumbu ya kuhuzunisha kwa Wacameroon na Waafrika, kufuatia kifo cha kiungo wa zamani wa Simba Wasiofungika, Marc Vivien Foe.
Foe alikuwemo kwenye kikosi cha Cameroon kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mabara mwaka 2003 nchini Ufaransa na akacheza katika mechi walizoshinda dhidi ya Brazil na Uturuki, kabla ya kupumzishwa kwenye mechi dhidi ya Marekani, kwa sababu tayari Simba Wasiofungika walikuwa wamekwishafuzu Nusu Fainali.
Juni 26, mwaka 2003, Cameroon ikapambana na Colombia katika mchezo wa Nusu Fainali Uwanja wa Stade de Gerland mjini Lyon, Ufaransa na dakika ya 72 ya mchezo, Foe alianguka katikati ya Uwanja na kupoteza fahamu, huku wachezaji wenzake wakiwa wamemzunguka.
Baada ya kuonekana tatizo lake ni kubwa, akatolewa kwa machela hadi nje ya Uwanja ambako alipatiwa tiba zaidi, madaktari wakitumia dakika 45 kujaribu kuokoa maisha yake, kabla ya kumhamishia zahanati ndogo ya uwanjani, ambako ndiko umauti ulimfika.
Michuano ya Kombe la Mabara hufanyika kila baada ya miaka minne, ikishirikisha mabingwa wa Mabara yote sita, UEFA, CONMEBOL, CONCACAF, CAF, AFC na OFC, pamoja na bingwa mtetezi wa Kombe la Dunia na mwenyeji wa fainali hizo kukamilisha idadi ya timu nane.
No comments:
Post a Comment