Kabla ya kupata neno la watoto hao, kufuatia kifo cha Sir Andy, kumekuwa na maswali mengi juu ya nini kinaendelea kwenye jamii hiyo kwa sasa hivyo Wikienda lilijipa kazi ya kutafuta majibu ya maswali.
NINI KINAENDELEA FREEMASON?
Katika nusanusa yake, Wikienda lilifika kwenye Hekalu la Freemason lililopo Mtaa wa Sokoine, mkabala na Hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro jijini Dar, jirani na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kutaka kujua kinachoendelea kwa kujigeuza mhitaji wa kujiunga na jamii hiyo.
Gazeti hili lilipofika mahali hapo mishale ya mchana, hakukuwa na pilikapilika nyingi zaidi ya mama ntilie aliyekuwa akisubiria wateja wa msosi.
Baada ya kuona kimya, ‘pandikizi’ wetu alijaribu kuzama ndani, lakini kabla ya kuvuka geti ambalo lilikuwa wazi kwenye mlango mdogo, alikutana na mlinzi aliyemhoji alikokuwa anakwenda.
Mlinzi: Haloo unakwenda wapi?
Wikienda: Samahani, nataka kuingia ndani kuulizia ‘process’ za kujiunga na Freemason, kwani hapa si ndilo hekalu lao?
Mlinzi: Ndiyo ni hapa, lakini hakuna shughuli ya watu kujiunga kwani nani amekuambia watu wanajiunga?
Wikienda: Sasa kwa mtu anayehitaji kujiunga inakuwaje?
Mlinzi: Hapa hakuna hilo zoezi na wala hakuna mtu aliyewahi kuja hapa akaunganishwa na Freemason. Kama yupo, huyo alitapeliwa tu maana mjini shule.
Wikienda: Inamaana wenyewe hawapo au?
Mlinzi: Wenyewe hawapo, mara ya mwisho sikumbuki vizuri labda ilikuwa mwezi wa tatu, lakini kuanzia mwezi ujao (wa saba) watakuwepo.
Wikienda: Sasa kama hivi nataka kujiunga, inakuwaje?
Mlinzi: Kwanza unataka kujiunga na nini na ili iweje?
Wikienda: Nataka kujiunga na Freemason. Nasikia watu waliojiunga wanapata pesa nyingi na mimi ninazitaka bwana au wewe hutaki pesa ndugu yangu?
Mlinzi: Kweli wajinga ndiyo waliwao, yaani pamoja na ujanja wote unaamini kuna pesa za hivihivi bila kufanya kazi? Nimekuambia hapa hakuna ishu ya watu kujiunga wala sijawahi kuona watu wanakuja tu na kuunganishwa. Kama nilivyokuambia, kama kuna mtu aliunganishwa kwa kuja tu hapa ujue alitapeliwa.
Wikienda: Sasa, mbali na hapa, naweza kujiungia wapi kwingine?
Mlinzi: Mimi kwa hapa sijui, lakini nasikia makao yao makuu kwa Afrika Mashariki yapo Mombasa (Kenya). Sasa kama unataka uende huko kama una uwezo, lakini kwa hapa hakuna kitu kama hicho. Kwanza ninavyojua mimi, hayo ni mambo ya siri. Huwezi kuja hapa tu, ukasema unataka kujiunga, kivipi?
Baada ya mazungumzo hayo, mlinzi huyo alitaka kuwa mkali kwa kumuona pandikizi wetu kuwa ni ‘bogas’ hivyo pandikizi huyo aliondoka kwa maelezo kwamba, hakuna zoezi la watu kuunganishwa mahali hapo.
TURUDI KWA WATOTO WA SIR CHANDE
Katika mazungumzo yao na waandishi wetu, watoto wa Sir Chande, Manish Jayantilial na Rupean Jayantilial walieleza kinachoendelea kwenye jamii hiyo.
Manish alisema kuwa, kwa upande wake, yeye ni muumini wa Jumuiya ya Freemason kwa muda mrefu na malengo yake ni siku moja kuwa kiongozi mkubwa wa jamii hiyo.
“Ni jambo zuri mno, ni jamii ya watu wanaosaidiana duniani, nimekuwa member (mwanachama) wake kwa muda mrefu sana na ninatamani siku moja niwe kiongozi wake mkubwa,” alisema Manish kwa lafudhi ya Kihindi.
MIAKA MITATU BILA MAFANIKIO
Kwa upande wake, Rupean alikiri jamii hiyo kuendelea na shughuli zake mbalimbali duniani ikiwemo hapa nchini na kwamba anatamani mno kujiunga na Freemason.
Rupean alisema kuwa, kwa muda wa miaka mitatu sasa, amekuwa akifanya maombi ya kujiunga bila mafanikio lakini anaamini ipo siku naye atafuzu kama ndugu yake, Manish.
Alisema kuwa, sababu ya kushindwa kufuzu ni kwamba, bado hajatimiza masharti yanayotakiwa lakini anaamini siku akiyatimiza atakuwa mwanachama wake.
WALIVUTIWA NA BABA YAO
Manish na Rupean walisema kuwa, baba yao ndiye aliyewavutia kujiunga na Freemason kwa kuwa ni jambo zuri kuwa na jamii ya kusaidiana na kuwasaidia wenye shida mbalimbali kwa kujitolea.
Hata hivyo, walimalizia kwa kusema kuwa, mbali na Tanzania, pia wanaishi nchini Canada na India.
Sir Chande ambaye mwili wake ulichomwa moto kwenye Makaburi ya Baniani yaliyopo Makumbusho jijini Dar aliacha watoto watatu na wajukuu watatu.
Source: Global Publisher
No comments:
Post a Comment