Awali mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kusini, aliwasili kituoni hapo saa 6.00 mchana kwa ajili ya mahojiano.
Alikwenda kituoni hapo akiwa na Mratibu wa Uhusiano na Mawasiliano wa Chadema Mkoa wa Dar es Salaam, Tambwe Hiza na mawakili wa Kampuni ya Phoenix Advocates.
Mahojiano hayo na polisi yaliyodumu zaidi ya saa tano yalichukua sura mpya baada ya mbunge huyo kuwekwa ndani wakati akisubiriwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Ronald Makona ambaye hakuwapo kituoni hapo.
Akizungumza kituoni hapo, Tambwe alisema hatua ya kumkamata mbunge huyo inaweza kufifisha kampeni za udiwani ambazo zilipangwa kufanyika kesho katika Jimbo la Ruangwa mkoani Lindi.
Kuhusu hoja ya uchochezi, alisema katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni wa Kata ya Reli mkoani Mtwara hakukuwa na viashiria vyovyote vibaya kwa kuwa ulikuwapo usalama wa kutosha.
“Jana tulifika mkutanoni tulimaliza salama lakini tukiwa njiani kwenda Tandahimba mbunge alipigiwa simu na polisi wakimuhitaji.
“Lakini yeye aliwaahidi leo ndiyo ameafika lakini hadi sasa hatuoni dalili ya kuachiwa kwake,” alisema.
Mwanasheria wa Kampuni ya Phoenix Advocates, Rainery Songea alisema polisi wanadai mbunge huyo alitamka maneno ya uchochezi wakati wa uzinduzi wa kampeni katika Kata ya Reli Manispaa ya Mtwara Mikindani.
“Kimsingi wanamhoji kwa tuhuma za uchochezi ambazo wanasema jana akiwa kwenye kampeni za udiwani Kata ya Reli kuna maneno alitamka ambayo yanaweza kusababisha wananchi kufanya makosa,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya hakuweza kupatikana kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
No comments:
Post a Comment