Na Mustafa Ismail
Huku ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Dodoma umefikia
asilimia 100, kumekuwa na ongezeko la
ndege zinazotua kila siku kutoka ndege tatu hadi kufikia tisa.
Akizungumza wakati wa mahojiano, Meneja wa Kiwanja cha
Ndege cha Dodoma, Julius Mlungwana ameisema kukamilika kwa ukarabati huo
kutawezesha mashirika mengi ya ndege kuanza safari zake kuja Dodoma na hivyo
kupunguza gharama za nauli.
Mlungwana alisema ukarabati huo umekamilika Septemba 2,
mwaka huu na kina uwezo wa kuhudumua ndege zenye uwezo wa kubeba hadi abiria
90.
“Uwanja umekamilika kwa asilimia 100 kwa lengo la msingi na
kilichobakia ni kuweka alama tu,” alisema meneja huyo na kuongeza kuwa kwenye
usafiri wa anga kuna wadau wanaotumia kiwanja wakiwemo wafanyabiashara,
wafanyakazi wa umma, mawakala wa utalii, taasisi za kimataifa na serikali,
taasisi zisizo za kiserikali na wananchi.
“Hao wote wanatumia usafiri wa anga kilio chao kikubwa,
nauli za ndege ni kubwa,” alisema na kuongeza kuwa kilio cha wadau kwenye
usafiri wa anga ni gharama kubwa za usafiri kutokana na kuwepo kwa ndege mbili
zilizo kwenye ratiba ya usafiri ambazo ni Auric Air na Flight Link ambazo zina
uwezo wa kubeba abiria 13 kila moja.
“Pia kuna ndege zisizo na ratiba na za viongozi ambazo hazipo
kwenye mpangilio pamoja na mashirika ya kimataifa ambao wamekuwa wakitumia
ndege za kukodi,” alisema.
Naye Meneja Mradi wa Upanuzi wa uwanja huo kutoka Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mbila Mdemu alisema mara ya mwisho ukarabati
wa uwanja huo ulifanyika mwaka 1976, na 2005 ulifanyika upembuzi yakinifu kwa
ajili ya ukarabati, lakini upatikanaji wa fedha umekuwa ni kikwazo na usanifu
ukaishia kwenye ukarabati.
Alisema kutokana na agizo la Rais John Magufuli kuhamia
Dodoma, uwanja ulianza kufanyiwa ukarabati.
Awali ujenzi ulitakiwa kukamilika ndani ya miezi sita na
kuliwekwa malengo mawili ambapo ilitakiwa hadi Julai 20, mwaka huu kiwanja kiwe
na uwezo wa kuhudumua ndege zenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 70 na 90. Pia
hadi Agosti 31, mwaka huu kazi za msingi zote ziwe zimekamilika na kazi zote
zimefanikiwa kukamilika.
No comments:
Post a Comment