JOSE MOURINHO na Zlatan Ibrahimovic wamesimama kidete na kutaka Watu wampe Wayne Rooney heshima anayostahili.
Fowadi wa Manchester United, Zlatan Ibrahimovic, amesema Kepteni wa Timu yao, Wayne Rooney, ni Mchezaji Bora sana na anahitaji kuheshimiwa zaidi hasa baada ya Alhamisi Usiku kuivunja Rekodi ya Man United ya Kufunga Bao nyingi katika Mashindano ya UEFA Barani Ulaya.
Rooney ndie alifunga Bao la Kwanza wakati Man United inaiwasha Feyenoord ya Holland 4-0 katika Mechi ya Kundi A la UEFA EUROPA LIGI.
Bao nyingine za Man United zilifungwa na Juan Mata, Jesse Lingard na moja Kipa wa Feyenoord, Brad Jones, kujifunga mwenyewe alipopigwa tobo na Zlatan Ibrahimovic.
Rooney sasa ana Bao 39 Ulaya akifuatiwa na Ruud van Nistelrooy mwenye 38.
Pia Bao hilo limemfanya Rooney awe na Bao 248 kwa Man United akiwa Bao 1 tu nyuma ya Mshikilia Rekodi ya Ufungaji Bora katika Historia ya Klabu hiyo, Sir Bobby Charlton, ambae sasa ni Mkurugenzi hapo Man United.
Ibrahimovic, alietengeneza Bao hilo la Rooney, ameeleza: “Ni Mtu safi sana. Nina furaha amevunja Rekodi. Nitamsaidia kupata 1 zaidi. Hiyo ndio naona ni Rekodi ya kweli!”
Kwa kipindi hiki, Rooney amekuwa akisakamwa baada ya Gazeti moja la Udaku huko England kutoa Picha za Rooney alizopigwa na Mashabiki waliokuwa kwenye Harusi zikimwonyesha akiwa ‘chakari’ kwenye Hoteli waliyofikia Wachezaji wa Timu ya Taifa ya England Wiki 2 nyuma wakiwa Kambini kwa Mechi ya Kimataifa.
Rooney aliomba radhi kwa Picha hizo licha kupigwa Siku Wachezaji wa England kuwa Ofu na kisha kuwajibu wanaosamkama kuwa hawamuheshimu.
Baada ya Mechi hiyo na Feyenoord, Ripota mmoja alikumbushia tena ishu hiyo ya Picha na Rooney kukumea: “Hayo yote yamebuniwa na Watu kama wewe, mnakuza jambo ambalo si la msingi!”
Na Ibrahimovic ameeleza: "Inabidi tumthamini sana kama Mchezaji kwa yote aliyofanya. Sioni Wachezaji wengi England walivyofanya kama yeye. Lazima wamuheshimu zaidi!”
Nae Meneja wa Man United Jose Mourinho amesema: “Mtu kama yeye hapaswi kujibu hayo, mwacheni ale raha katika Miaka yake iliyobaki kwenye Soka!””
Mourinho aliongeza: “Rekodi ya Rooney ni ya kushangaza na itakuwa kitu kikubwa zaidi akiisaidia Klabu kutwaa Kombe pekee ambalo Man United hawajawahi kulibeba!”
Man United wamebeba Ubingwa wa Ulaya mara 3 na Kombe la Washindi Barani Ulaya mara 1 lakini hawajawahi kutwaa Kombe hili la UEFA EUROPA LIGI ambalo awali lilitwa UEFA CUP.
No comments:
Post a Comment