WACHEZAJI wa Simba SC wanatarajiwa kukutana leo Uwanja wa Chuo cha Polisi, Kurasini,Dar es Salaam kujipanga kwa ajili ya kuanza mazoezi ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Katibu Mkuu wa Simba SC, Patrick Kahemele alisema jana katika mazungumzo na Bin Zubeiry Sports - Online kwamba wachezaji hao watakutana chini ya Kocha Msaideizi, Mganda, Jackson Mayanja.
Alisema mazoezi rasmi yataanza Jumatano kwenye viwanja hivyo vya Polisi kwa kupokezana na mahasimu wao, Yanga SC ambao wamenza jana asubuhi.
“Mkutano wa leo utahusisha wachezaji ambao wanaishi Dar es Salaam pekee wakati tunasubiri wachezaji zaidi wakiwemo wa nje ya mji nan je ya nchi wawasili. Mazoezi yataanza rasmi Jumatano,”alisema Kahemele.
Aidha, Katibu huyo alisema kwamba kocha Mkuu, Joseph Marius Omog anatarajiwa kufika mwishoni mwa wiki kuanzisha programu kamili ya maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
Simba SC ilimaliza mzunguko wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa kileleni kwa pointi zake 35, mbili zaidi dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC.
No comments:
Post a Comment