Baada ya Chama cha Wananchi (CUF) upande wa Maalim Seif, kufungua ofisi mpya za chama hicho katika eneo la Mtaa wa Idrisa Kata ya Mzimuni, Magomeni wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, Msajili wa Vyama vya Siasa amesema anaamini chama hicho kinafanya mambo yake kwa kuzingatia sheria.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi,amezungumza na gazeti la Habarileo, ambapo alisema hajapata taarifa yoyote ya chama hicho, kufungua ofisi mpya zaidi ya kuona katika vyombo vya habari.
“Ukiondoa taarifa za kwenye media sijapata taarifa yoyote kutoka CUF labda wawe wameleta leo (jana), lakini naamini chochote wanachofanya wanaelewa taratibu wataleta taarifa,”alisema Jaji Mutungi.
Jaji Mutungi alisema sheria inawataka wanapofungua ofisi watoe taarifa ndani ya siku 14, ambazo hazijaisha hivyo anaamini wanajua hilo. Upande wa Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad wamefungua ofisi hizo, baada ya tukio la kuvamiwa katika Ofisi Kuu za Buguruni na kundi la Profesa Ibrahim Lipumba.
Jaji Mutungi alisema atakapopokea taarifa rasmi ataangalia kama taratibu zikifuatwa kwani ufunguaji wa ofisi mpya una taratibu zake. “Nikiletewa taarifa ndio nitajua kama walifata taratibu au la, ufunguaji wa ofisi una taratibu zake najua wanazijua pia,” alisema Jaji Mutungi.
No comments:
Post a Comment