Aua mke kwa wivu wa mapenzi - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Tuesday, August 15

Aua mke kwa wivu wa mapenzi


Singida. Watu wawili wamefariki dunia mkoani Singida katika matukio tofauti likiwemo la mwanamke kudaiwa kuuawa na mume wake kutokana na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa.

Mwanamke huyo Sele Shija (34) amefariki dunia baada ya kupigwa kwa  fimbo kubwa kichwani na sehemu mbalimbali za mwili na mume wake Gyuda Jackson (35) wote ni wakazi wa Kijiji cha Ntwike tarafa ya Shelui wilayani Iramba.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida,Debora Magiligimba alisema tukio hilo limetokea Agosti 14 mwaka huu saa 7.40 mchana katika Kijiji cha Ntikwe.

Alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni wivu wa kimapenzi baada ya Gyuda kuhisi mke wake Sele ana mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa.

“Hisia hizo zilisababisha ugomvi baina ya wana ndoa hao na kusababisha Gyuda kufunga mlango ili majirani wakose nafasi ya kuamua ugomvi huo. Wakati wakiendelea kugombana Sele (marehemu) alimzidi nguvu mume wake. Kitendo hicho kilisababisha Gyuda achukue fimbo kubwa na kumpiga kichwani na kusababisha jeraha kubwa. Jeraha hilo lililosababisha atokwe na damu nyingi na kufariki papo hapo,”alifafanua Kamanda.

Kamanda Magiligimba alisema kwa sasa wanamshikilia Gyuda kwa ajili ya upelelezi zaidi na mara utakapokamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma ya kumuua mke wake.

Katika tukio la pili kamanda huyo alisema mchimbaji dhahabu katika mgodi wa Sekenke One Kitongoji cha Nkonkilangi wilayani  Iramba, Msafiri Matiko (21) amefariki dunia Agosti 13 mwaka huu saa moja usiku.

Alisema kuwa Msafiri wakati akitoka kwenye shimo duara namba 38B yeye na wachimbaji wengine sita aliteleza kwenye ngazi na kutumbukia ndani ya shimo kitu kilichomsababishia kupata majeraha makubwa.

Magiligimba alisema wachimbaji wenzake waliweza kumtoa nje ya  shimo hilo lakini alifariki dunia akiwa njiani akipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Iramba kwa matibabu.

“Jeshi la polisi linatoa wito kwa wamiliki wa migodi kuboresha mazingira na kuyaweka kiusalama kwa wafanyakazi wao. Pia wahakikishe kunakuwepo na vifaa stahiki vya kujikinga na madhara wakiwa ndani ya migodi,” alisema Kamanda Magiligimba.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here