Tukio hilo limeibua utata kutokana na hakimu huyo kuvamiwa nyumbani na kujeruhiwa kwa mapanga bila wahusika kuchukua mali yoyote.
Baada ya kujeruhiwa, Ulaya alikimbizwa kupata matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Masasi.
Kamanda wa Polisi mkoani Mtwara, Neema Mwanga, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa lilitokea juzi saa 2:30 usiku wakati hakimu huyo akiwa amelala nyumbani kwake maeneo ya Mtandi Kata ya Mtandi.
Kamanda Mwanga alisema kundi la watu watatu wakiwa na mapanga walivamia nyumba ya hakimu huyo kisha kuanza kuwasumbua watoto wake ambao walikuwa nje ya nyumba hiyo, na baada ya Ulaya kusikia sauti za watoto wake alitoka nje na kukutana na majambazi hao.
Alieleza wakati Ulaya akiwa katika jitihada za kuwaokoa watoto wake wakiwa mikononi mwa majambazi hao, walianza kumpiga kwa kutumia mapanga hayo na kumjeruhi katika maeneo mbalimbali ya mwili wake.
Alisema moja ya maeneo ambayo hakimu huyo amejeruhiwa vibaya ni mikono yote na kuwa hata hivyo, alifanikiwa kukimbia kisha majambazi hao walifanikiwa kutoroka.
Kamanda Mwanga alisema watu hao haijajulikana walikuwa na dhamira gani dhidi ya hakimu huyo na kwamba hawakuchukua mali yoyote ya hakimu huyo.
Mwanga alisema baada ya Ulaya kujeruhiwa, alikimbizwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Masasi kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Alisema hadi sasa hakuna mtu yeyote ambaye anashikiliwa na polisi kuhusiana na tukio hilo na kwamba Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi na atakayebainika kuhusika atafikishwa katika mkono wa sheria.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hispitali hiyo, Dk. George Kumwembe, alithibitisha kumpokea hakimu huyo akiwa na majeraha na kupatiwa matibabu ya awali.
Dk. Kumwembe alieleza kuwa hakimu huyo kutokana na hali yake kutokuwa nzuri, alipatiwa rufani na kupelekwa katika Hospitali ya Peramiho ya mjini Songea kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.
No comments:
Post a Comment