Kikosi cha Simba jana jioni kilitua Unguja, Zanzibar kwa ajili ya kunoa makali yake tayari kuwavaa mahasimu wao Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii utakaopigwa Agosti 23, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, kiongozi mmoja wa juu wa klabu hiyo (jina tunalihifadhi) alisema wakiwa Unguja wachezaji watakuwa wanafanya mazoezi kwa awamu tatu tofauti kwa siku.
Kiongozi huyo alisema mbali na mazoezi ya uwanjani, pia wataisoma Yanga kwa kuziangalia mechi mbalimbali ambazo imecheza kwa ajili ya kujipanga kuwakabili kwenye mchezo huo wa ufunguzi wa msimu huu wa 2017/2018.
"Hatuendi tena Morogoro, leo (jana) jioni tunaenda Zenji (Zanzibar)," alisema kwa kifupi kiongozi huyo.
Taarifa zaidi kutoka Simba zinasema kuwa ikiwa Zanzibar, kikosi chao kinaweza kucheza mechi mbili za kirafiki ambazo zitatokana na ushauri utakaoamuliwa na benchi la ufundi la timu hiyo lililoko chini ya Mcameroon, Joseph Omog.
"Tunajua ni mechi yenye changamoto nyingi za ndani na nje ya uwanja, tunaenda kujiimarisha na kufanya majumuisho ya mazoezi tuliyofanya kuanzia tulipoweka kambi Afrika Kusini," alisema kiongozi huyo.
Kwa upande wa Yanga ambayo ilitangulia kutua Zanzibar, Kocha wa timu hiyo, Mzambia George Lwandamina, amesema kwa asilimia 80 programu yake ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu imekamilika na kwa sasa anafanyia kazi baadhi ya kasoro ndogo alizoziona kwenye michezo ya kirafiki dhidi ya timu yake iliyocheza.
Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mazoezi ya asubuhi, Lwandamina, alisema kipo kitu ambacho alikuwa akikitafuta kwenye maandalizi yake na kwa sasa kikosi chake kimeiva.
“Kuna mambo mengi kwenye maandalizi ya msimu mpya, niwahakikishie Wanayanga kuwa tuna kikosi kizuri ambacho kitakuwa tayari kutetea ubingwa wetu pamoja na kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa,” alisema Lwandamina.
Aidha, alisema kuwa tofauti na watu wanavyochukulia, yeye hakuna timu anayoihofia na maandalizi ya timu yake si kwa ajili ya timu moja tu, bali anaiandaa kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye michezo yote ya Ligi Kuu pamoja na michuano ya kimataifa.
No comments:
Post a Comment