Ajali hiyo ilitokea Agosti 15 mwaka huu na katika tukio hilo, wanafunzi hao walikuwa wakichimba mchanga kwa ajili ya matumizi ya ujenzi wa darasa katika shule yao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Mwandamizi wa Polisi, Jemini Mushi aliwataja wanafunzi hao kuwa ni Sofia Ngongi na Semeni Selemani waliokuwa wakisoma darasa la tatu shuleni hapo.
Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Omary Melle, alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa 9.20 alasiri, wakati wanafunzi hao walipotoka madarasani baada ya muda wa masomo.
Alisema shule hiyo imekuwa ikiwatumia wanafunzi kusomba mchanga kutokana na baadhi ya wawazi na walezi wao kugoma kufanya kazi za kujitolea ili kufanikisha ujenzi wa madarasa shuleni hapo.
Wakisimulia mkasa huo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mbesa, Raso Kundete na Diwani wa Kata hiyo, Abdul Mfaume, walisema kuwa baada ya tukio hilo, wanafunzi hao walipiga kelele kwa ajili ya kuomba msaada lakini walitolewa wakiwa wameshakufa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ujenzi wa Shule hiyo, Mkape Nasoro, alisema walimu hao wamepewa ruhusa ya kuwatumia wanfunzi wao kubeba mchanga huo ili kuharakisha ujenzi wa darasa hilo.
Wakiongea kwa nyati tofauti baadhi ya wananchi wa Kijiji hicho, waliwatuhumu walimu hao kuwa wamekuwa na tabia za kuwatumikisha watoto wao.
Akifafanua taarifa hiyo, Mweneyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Chikomo, Mitawa Adam, alisema wanafunzi hao walianza kubebeshwa mchanga huo bila kutoa taarifa yoyote kwa viongozi.
Alisema wananchi wa kijiji chake ni wasikivu na ndiyo maana walikubali kujitolea kufyatua matofali ambayo kwa sasa yanatumiwa kwa ajili ya ujenzi wa darasa hilo.
Mganga aliyeifanyia uchunguzi miili ya wanfunzi hao, Dk. Andreas Ndunguru, alisema kuwa chanzo cha kifo hicho ni wanafunzi hao kukosa hewa baada ya kufunikwa na kifusi cha udongo huo.
No comments:
Post a Comment