Dar es Salaam. Watu wanane wanaodaiwa kuwa ni wahalifu wamevamia jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza na kufanya uharibifu wa mali za wapangaji.
Jengo la Prime House lina ghorofa tano lipo jirani na ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.
Mwandishi wa gazeti hili ameshuhudia barabara ya kuingia eneo hilo ikifungwa kwa muda na polisi ambao walitumia magari yao kuziba njia na kuweka uzio wa utepe wa rangi ya njano.
Jengo la Prime House lina ofisi za kampuni mbalimbali, zikiwemo za mawakili, duka la dawa na sehemu ya kufanya mazoezi gym.
Mmoja wa mawakili ambao wana ofisi katika jengo hilo, ambaye hakutaka kutaja jina lake aliliambia gazeti hili kwamba watu hao walipofika walimfunga mlinzi kwa kamba na kisha kuingia ndani kwa nguvu.
"Mlinzi ameniambia baada ya kuingia walipokuwa wakifanya upekuzi walikuwa wakisikika wakisema si huku tutazame ghorofa linalofuata si hili,” wakili huyo amemkariri mlinzi.
Wakili huyo amesema, "Sasa nipo njia panda sijui walikuwa wanalenga ofisi gani, kwa vyovyote hawawezi kwenda gym kuchukua vifaa kwa sababu ni vizito nadhani kuna ofisi waliilenga hadi sasa sijajua kwa sababu sijaingia ndani tumekatazwa kuingia."
Amesema wanasubiri uchunguzi wa polisi ambao wapo katika harakati za kuingia ndani ya jengo hilo kujua uharibifu uliojitokeza.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Salum Hamduni amethibitisha tukio hilo akisema limetokea kati ya saa nane na saa tisa usiku wa kuamkia leo.
"Kwa sasa siwezi kusema wahalifu hawa walilenga ofisi gani maana zipo nyingi katika jengo lile. Naomba mtupe nafasi tufanye uchunguzi kisha tutawapa taarifa," amesema Kamanda Hamduni
No comments:
Post a Comment