Mkwelitzblog
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati
MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati, amemwaga mtama kuhusu ukora uliofanywa na kamati simamizi ya tume hiyo wakati wa uchaguzi wa urais wa Agosti 8.
Kwenye barua kali aliyomwandikia Afisa Mkuu Mtendaji, Ezra Chiloba, Bw Chebukati amefichua mambo mengi yaliyokwenda kombo, ikiwemo kuibwa kwa nambari ya siri (pasiwadi) yake na kutumiwa mara 9,934 na watu asiowajua.
Nambari hiyo hiyo ilitumiwa kuingia kwenye mitambo ya kielektroniki ya IEBC kuvuruga matokeo ya urais, ambayo Mahakama ya Juu ilithibitisha hayakuwa halali.
“Nataka unieleze ni kwa nini mitambo ya kiteknojia iliyonunuliwa na tume kwa Sh848 milioni haikutumika kutuma matokeo ya uchaguzi kama ilivyopangwa,” akaandika Bw Chebukati katika barua yake iliyo na maswali 12 kwa Bw Chiloba.
Barua hiyo iliyoandikwa Septemba 5, inaeleza kwa kina utendakazi mbaya wa maafisa walio chini ya Bw Chiloba, uliopelekea Mahakama ya Juu kutupilia mbali uchaguzi wa urais.
Bw Chebukati anasema mitambo ya Kenya Integrated Elections Management System (KIEMS), ilitakiwa kutumika katika vituo maalumu. Kwa mfano kifaa cha kituo cha Shule ya Msingi ya Jomo Kenyatta kitumike katika shule hiyo pekee.
Ni kwa nini?
Lakini ilibainika kuwa, kinyume na kanuni hizo, kundi la Bw Chiloba lilitumia mitambo hiyo katika maeneo tofauti.
“Kwa nini baadhi ya KIEMS zilitumia huduma za Airtel na Telkom katika maeneo ambayo huduma za Safaricom zilihitajika pekee?” anauliza Chebukati katika barua hiyo.
Anataka pia afisi ya Bw Chiloba ieleze utata uliotokea katika vituo vya kupigia kura, hasa kuhusiana na idadi ya kura zilizokataliwa.
“Eleza ni kwa nini vituo 682 vya kupigia kura, idadi ya kura zilizokataliwa ilikuwa sawa na idadi ya wapigakura waliosajiliwa katika vituo hivyo.”
Mbona GPRS ilizimwa?
Hiyo ina maana kuwa kura zote za wapigakura katika vituo hivyo zilikataliwa.
Mwenyekiti huyo alitaka pia kujua ni kwa nini mitambo ya kufuatilia eneo la kifaa cha KIEMS (GPRS) ilizimwa siku tatu kabla ya uchaguzi kuanza. Ina maana kuwa IEBC haingeweza kujua matokeo yaliyotumwa na vifaa hivyo yalitoka kituo gani.
“Nataka maelezo kwa nini vituo 10,366 kati ya vituo vyote 40,883 vya kupigia kura havikutuma matokeo ya kura yakiandamana na fomu 34A,” anamuuliza Bw Chiloba.
Bw Chebukati pia alitaka maelezo kuhusu fomu mbazo hazikuwa na alama maalumu za kuthibitisha uhalali wake kuambatana na mkataba wa IEBC na kampuni ya Al Ghurair, iliyochapisha karatasi za uchaguzi.
Mgawanyiko
Barua hiyo, iliyoibua hisia kali miongoni mwa Wakenya inafichuka wakati ambao IEBC imegawanyika kuhusu hatua ya Bw Chebukati kuteua maafisa wapya kusimamia uchaguzi wa Oktoba 17.
Bw Chebukati alijipata njiapanda baada ya muungano wa NASA na chama cha Jubilee kupuuza uteuzi wa maafisa hao wapya na kutaka mashauriano ya kina kufanywa kabla ya maamuzi muhimu kufanywa katika tume yake.
Hata hivyo, Bw Chebukati alipuuza matakwa ya vyama vya kisiasa kuhusu uteuzi huo akivitaka viheshimu uhuru wa tume hiyo.
No comments:
Post a Comment