Ofisa kilimo achapwa bakora na wakulima - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Tuesday, September 12

Ofisa kilimo achapwa bakora na wakulima



Igunga. Zaidi ya wakulima 19 waliovamia vyanzo vya maji katika bwawa la Mwanzugi wilayani Igunga Mkoa wa Tabora, wamemchapa bakora Ofisa Kilimo wa Kata ya Igunga, Jamila Issa kwa kuwapiga picha.

Tukio hilo lilitokea juzi wakati ofisa huyo alipokwenda kuangalia utekelezaji wa agizo la siku 14 alilolitoa Agosti 27 kuwataka wakulima hao wawe wameondoka katika bwawa hilo.

Ofisa huyo alisema alikwenda eneo hilo akiwa amefuatana na baadhi ya viongozi wa mtaa kukagua iwapo wakulima wameondoka, lakini waliwakuta wakiendelea na kilimo kwenye vyanzo vya maji. “Nilipofika eneo hilo nilikuta wakulima zaidi ya 19 wakiendelea na kilimo, baadhi wakipanda nyanya na mahindi. Nilianza kuwapiga picha kupata ushahidi, walipobaini walinishambulia kwa fimbo huku viongozi niliofuatana nao wakitimua mbio,” alisema ofisa kilimo, Jamila.

Alisema baada ya kuanguka, wakulima walitimua mbio na majembe yao na fahamu zilipomrudia alienda kituo cha polisi kuchukua fomu kwa ajili ya matibabu ambayo aliyapata katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga na aliruhusiwa kurejea nyumbani.

Hata hivyo, alisema hataogopa kufanya kazi na kuwachukulia hatua wote watakaoendelea kulima kwenye vyanzo vya maji.

Mtendaji wa Kata ya Igunga, Robert Mwagala amesema Polisi kwa kushirikiana na raia wema watawasaka wakulima waliomshambulia ofisa kilimo huyo.

Diwani wa Igunga, Charles Bomani alisema kitendo kilichofanywa na wakulima hao hakikubaliki, hivyo ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Baadhi ya wakulima waliotii agizo la kuondoka kwenye bwawa hilo wameliomba Jeshi la Polisi kuchukua hatua za haraka juu ya watu waliofanya ukatili huo.

Mkazi wa Kata ya Igunga, Idd Jackson alisema ni aibu na fedheha kumshambulia kiongozi akitekeleza majukumu yake, hivyo ni lazima hatua za kisheria zichukuliwe kwa waliohusika.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here