Wawili Wauawa kwa Ushirikina - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Wednesday, January 31

Wawili Wauawa kwa Ushirikina



Watu watatu wameuawa katika matukio tofauti likiwamo la wanawake wawili kuuawa kwa kukatwa mapanga kutokana na imani za kishirikina.

Tukio la kuuawa wanawake hao lilitokea usiku wa kuamkia jana kitongoji cha Kilombero, Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando aliwataja waliouawa kuwa ni Salome Kisinza (50) na Rahel Pawa (22) ambao walikatwa mapanga sehemu mbalimbali za miili yao na watu wasiojulikana.

Kyando alisema waliofanya mauaji hayo waliwavizia wakiwa wamelala ndani ya nyumba yao, walivunja mlango na kuingia ndani na kuanza kuwakata mapanga.

Alisema walimuua Salome na kumjeruhi Rahel baadaye walitoweka, huku wakimwacha katika hali mbaya na alifariki dunia njiani akipelekwa hospitali.

Kamanda Kyando alisema chanzo cha mauaji hayo inasadikiwa ni tuhuma za imani za ushirikina kwa kuwa Salome alikuwa akituhumiwa kumroga mume wake, Jilala Mponeja ambaye amekuwa akiumwa kwa muda mrefu na anatibiwa kwa mganga wa jadi wilayani Kalambo mkoani humo.

Katika tukio jingine lililotokea saa tatu usiku kwenye Sekondari ya Tawheed Manispaa ya Sumbawanga, mtu aliyefahamika kwa jina moja la Hassan (27) mkazi wa Kizwite aliuawa kwa kipigo akituhumiwa kwa wizi.

Alisema Hassan alikuwa anatuhumiwa kuiba bomba moja la chuma na misumari kilo moja na nusu, ambavyo thamani yake haijajulikana.

Alisema watuhumiwa wa mauaji hayo alimfungia Hassan ndani ya stoo kisha kumpiga sehemu mbalimbali za mwili wake hadi alipofariki dunia.

Kamanda Kyando alisema watuhumiwa sita wa mauaji hayo akiwamo mlinzi wa stoo, mwalimu wa Sekondari ya Tawheed na wanafunzi wanne wanashikiliwa kwa mahojiano na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.   

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here