Huku vifo vya waathirika wa tetemeko la ardhi
mkoani Kagera vikiongezeka na kufikia 17, uongozi wa mkoa huo umesema
zinahitajika zaidi ya Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya mahitaji mbalimbali ya
waathirika, na tayari serikali jana imehamasisha na kupatikana zaidi ya Sh
bilioni 1.4.
Kati ya fedha hizo zilizopatikana, Sh milioni 700 zilikuwa
ahadi, fedha taslimu Sh milioni 646, Dola za Marekani 10,000, Euro 10,000 na
mifuko 2,800 ya saruji.
Kampuni za mafuta ya Oilcom, GBP na Moil, zimejitolea
kujenga shule mbili za sekondari zilizoathiriwa na tetemeko hilo. Shule hizo
zimefungwa. Jumamosi iliyopita, saa 9.27 alasiri mji wa Bukoba ulikumbwa na
tetemeko la ardhi, ambalo nguvu ya mtetemo wake ulikuwa ni 5.7 kwa kutumia
skeli ya “Ritcher”.
Ukubwa huo ni wa juu kiasi cha kuleta madhara makubwa
ikiwemo kuanguka nyumba, nyingine zimepata nyufa, watu 17 wamekufa, na mamia
wawamejeruhiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Salum Kijuu alisema, baada ya Kamati
ya Maafa ya Mkoa na Kamati ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama, wamefanya tathmini ya haraka na kubaini mahitaji kwa
wananchi walioathirika.
Alitaja mahitaji ya muhimu ambayo yanahitaji kwa haraka ni
dawa, tiba na vifaa tiba, vifaa vya ujenzi mabati 90,000 yenye gharama ya Sh
bilioni 1.7, saruji mifuko 9,000 yenye thamani ya Sh milioni 162, mbao zenye
thamani ya Sh milioni 450 na misumari yenye thamani ya Sh milioni 12 ambapo
jumla ni Sh bilioni 2.3. Majaliwa achangisha bil 1.4/- Wakati Kijuu akisema
hayo, Majaliwa amehamasisha wafanyabiashara pamoja na mabalozi, kuchangia na
kuchangisha zaidi ya Sh bilioni 1.4.
Katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam,
Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa kutokana na tetemeko hilo kubwa, imelazimu
serikali kuzifunga shule mbili za sekondari zilizoharibiwa vibaya za Nyakato na
Ihungo. Waziri Mkuu alisema tetemeko hilo ni kubwa ambalo halijawahi kutokea
nchini, hivyo haikutarajiwa na wala hakukuwa na maandalizi ya kukabiliana na
hali kama hiyo.
Alisema mpaka jana watu 17 walikuwa wamefariki dunia huku
253 wakijeruhiwa na 145 walikuwa wako katika hospitali huku vitu vingi pamoja
na miundombinu vikiharibika.
Katika miundombinu ya shule nne za Nyakato, Ihungo, Kashenge
na Buhembe, zimeharibika ikiwemo vyoo, nyumba za walimu, kumbi za shule na
mabweni yameharibika kabisa pamoja na hospitali na vituo vya afya navyo
vimeharibika.
Alisema kuna baadhi ya sehemu hali ni mbaya na wanahitaji
msaada ambapo nyumba 840 zimeanguka kabisa chini huku nyumba na majengo 1,264
yakiwa na nyufa na kamati ya maafa katika mkoa pamoja na viongozi wake
wanaendelea kufanya tathmini ya kiasi cha hasara iliyopatikana.
Alisema serikali imefanya juhudi katika kukwamua maisha ya
wananchi wake na mawaziri watatu wako mkoani humo kuangalia namna ya kukabiliana
na majanga hayo ambao ni Waziri wa Ujenzi, Profesa Makame Mbarawa, Elimu
Profesa Joyce Ndalichako na Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista Mhagama.
Alisema kupitia kitengo cha maafa katika Ofisi ya Waziri
Mkuu wamefungua akaunti hiyo katika benki ya CRDB huku wakiendelea na
maandalizi ya kupata namba za kuchangia kwa simu ya mkononi huku akiwashukuru
wabunge walioamua kuchangia maafa hayo kwa kutochukua posho zao za siku ya
jana.
Mabalozi, Wafanyabiashara Mkuu wa Jumuiya ya Mabalozi,
Balozi wa Zimbabwe nchini, Edzai Chimonyo alisema kutokana na tarifa hiyo kuwa
ya ghafla na wako sehemu mbalimbali duniani watakusanyika na kuwasilisha
michango yao. Lakini, hata hivyo, balozi mbalimbali zilijitokeza kuwasilisha
michango yao ikiwemo Ubalozi wa China, uliotoa Sh milioni 100, wafanyabiashara
wa Kichina walitoa Sh milioni 100 na Ubalozi wa Kuwait Sh milioni 50.
Pia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, ilitoa mchango wa wafanyakazi wake Sh milioni 10 huku ikiandaa
matembezi ya kuchangisha fedha zaidi kwa waathirika wa tetemeko hilo
yatakayofanyika Jumamosi wiki hii. Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Azizi Mlima
alisema wameanza kwa kukabidhi fedha hizo ambazo ni mchango wa wafanyakazi,
lakini Jumamosi wamealika wadau mbalimbali katika matembezi hayo
watakayochangia zaidi.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),
Reginald Mengi alisema wafanyabiashara wako pamoja katika kuhakikisha
wanakabiliana na tatizo hilo na kuipongeza serikali kwa hatua za haraka
walizochukua kukabili majanga hayo.
Mengi alichangia Sh milioni 110, Kampuni ya Mohammed
Enterprises (MeTL) kupitia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wake, Mohamed Dewji ilitoa
Sh milioni 100, Kampuni ya Bia (TBL) Sh milioni 100, Chama cha Wauzaji Mafuta
kwa Rejareja Sh milioni 250 huku Umoja wa Waagizaji Mafuta ukiahidi kuchangia
baada ya kikao watakachokaa leo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Viwanda, Biashara
na Uwekezaji, Charles Mwijage alishukuru kwa wafanyabiashara na mabalozi kwa
michango hiyo na kuomba ipatikane kwa haraka ili kusaidia wananchi wa mkoa huo
kurejea katika maisha yao ya kawaida.
No comments:
Post a Comment