WAPIGA DILI KIKAANGONI - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Tuesday, December 13

WAPIGA DILI KIKAANGONI

Na Mustafa Ismail
SERIKALI imeendelea kuwabana wapiga ‘dili’ na vishoka wanaotumia ujanja kujinufaisha kupitia michakato ya manunuzi ya umma na kuwataka waache mara moja kwa sababu haitawavumilia pindi itakapowabaini.


Naibu waziri wa fedha na mipango Dk Ashatu kijaji
Akizungumza katika kongamano la saba la wataalamu wa Bodi ya Manunuzi na Ugavi linalofanyika mkoani hapa, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji, alisema ni vizuri kila mhusika wa manunuzi asimame vizuri kuhakikisha kila fedha inayotoka ya serikali inakwenda kufanya kazi iliyokusudiwa.
“Nataka wataalamu muelewe, wote waliozoea kupiga ‘dili’ na vishoka sasa basi na hatutaki kuona hilo na tutafuatilia kila fedha inayotoka kuhakikisha inafanya jambo la maendeleo kusudiwa,” alisema.
Dk Kijaji alisema serikali imetenga asilimia 40 ya bajeti kwenda katika miradi ya maendeleo na ndani na asilimia 70 ya fedha hizo zinakwenda kwenye manunuzi ya maendeleo, hivyo lazima kusimamia vizuri eneo hilo.
Alisema hawatamvumilia mtu yeyote atakayekwenda vibaya katika manunuzi au mchakato mzima wa manunuzi na hata waliozoea kupewa asilimia 10 waache mara moja.
“Hizo asilimia kumi hatutaki kusikia wala kuona, mmezoea, acheni mara moja maana hamtabaki salama, tunataka kuona kama Sh 100 inakwenda barabarani, iende yote. Ukaguzi utafanyika na kufanya tathmini kuona kama fedha zote hazijaishia kwa vishoka na ‘wapiga dili’,” alisema.
Aidha, alisisitiza kuwa wataalamu wanapaswa kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania, ili viwanda vilivyokusudiwa vijengwe kweli, lakini kukiwa na watu wajanja wajana hakutakuwa na viwanda na serikali haipo tayari kuona inaangushwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Manunuzi na Ugavi (PSPTB), Dk Hellen Bandiho, alisema wenye mazoea ya kupiga dili waache mara moja kwa sababu wakiendelea nayo watakufa nayo.
“Tunataka kila mmoja afanye kazi kwa kufuata maadili, kama umepewa zabuni itumike ipasavyo na ukipatiwa fedha na serikali ifanye kazi iliyokusudiwa. Alisema tutahakikisha wanaofanya manunuzi ya serikali wanakuwa watu wenye sifa na ikigundulikana mtu anakwenda kinyume na sheria kama tunavyotaka, sheria itachukua mkondo wake,” alisema Dk Bandiho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here