Mchezaji soka wa kimataifa amefanya ziara ya kihujaji kwenda katika mji mkatatifu zaidi wa Kiislamu, Mecca, wakati wa mwanzo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mchezaji huyo ambaye ni raia wa Ufaransa Paul Pogba alipakia mtandaoni picha yake akiwa Mecca siku ya Jumapili na kuandika "kitu cha kupendeza zaidi nilichowahi kukitazama maishani mwangu."
Aidha, aliandika ujumbe kwenye Twitter kutakia kila mtu "Ramadhani jema."
Pogba, 24, aliibuka mchezaji ghali zaidi katika historia majira ya joto mwaka jana, Manchester United walipowalipa Juventus ada ya £89m ($114m).
Jumatano, alifunga bao na kusaidia Manchester United kulaza Ajax 2-0 na kushinda kombe la ligi ndogo ya klabu Ulaya, Europa League mjini Stockholm, Sweden na pia kuwezesha klabu hiyo kufuzu kwa Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.
Baada ya kumalizika kwa msimu wa soka, Pogba alipakia mtandaoni video fupi yake na mkoba na kusema alikuwa "safarini" kwenda kufanya maombi yake.
Pogba anafanya Umrah, ambayo ni safari ya kihujaji ambayo si ya lazima katika dini ya Kiislamu.
Pogba amewahi kuzuru Mecca angalau mara moja awali, ambapo alifanya Haji, safari ya kihujaji ambayo kila Mwislamu aliyekomaa na mwenye afya anafaa kuifanya angalau mara moja maishani.
Mecca unaaminika kuwa mji alikozaliwa Nabii Muhammad, na watu wasio Waislamu hawaruhusiwi kuingia.
source:bbc swahili
No comments:
Post a Comment