Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 29, mwaka 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa imesema Dk Slaa amemshukuru Rais kwa kumteua kuwa Balozi na kuahidi kuwa yupo tayari kutekeleza majukumu atakayopangiwa kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.
Imeeleza kuwa Dk Slaa ameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa uongozi bora na kutekeleza mambo makubwa ikiwemo miradi ya ujenzi wa reli ya kisasa, ujenzi wa daraja la juu katika makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela, mradi wa uzalishaji umeme katika maporomoko ya mto rufiji na mapambano dhidi ya rushwa.
“Kwa kweli naona faraja, ninafurahi Serikali ya Awamu ya Tano inatekeleza hatua kwa hatua karibu yote tuliyokuwa tunayapigania kwa miaka takribani 20 ya huko nyuma, mimi Dk Slaa nilikuwa napiga kelele kwa sababu nilikuwa naona kuna upungufu,” imesema taarifa hiyo ikimnukuu Dk Slaa.
Kwa upande wake, Rais Magufuli amempongeza daktari huyo kwa moyo wake wa kizalendo na amesema aliamua kumteua kuwa Balozi kwa kuwa anatambua ataweza kupigania maslahi ya Tanzania popote atakapopangiwa kuiwakilisha.
“Dk Slaa alinijulisha kuwa anakuja na akaomba akija angependa kuja kuniona na nikampangia leo, tumezungumza mambo mengi na ameniahidi kuwa atakwenda kufanya kazi yake vizuri kwenye nchi atakayokwenda kuwa Balozi,” amesema Rais Magufuli na kuongeza,
“Mheshimiwa Dk Slaa ni mtu safi, anazungumza kutoka moyoni na anaipenda Tanzania na mimi kutokana na moyo wake wa kuchukia ufisadi na kuchukia wizi nikaamua kumteua kuwa Balozi.”
Wakati huohuo, Rais Magufuli ameagana na maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambao wamestaafu baada ya kutimiza umri.
Walioagana na Rais ni Luteni Jenerali James Mwakibolwa aliyekuwa Mnadhimu Mkuu wa JWTZ na Meja Jenerali Michael Isamuhyo aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Wengine ni Brigedia Jenerali Aron Lukyaa, Brigedia Jenerali Willima Kivuyo, Brigedia Jenerali Elizaphani Marembo na Kanali Peter Samegi.
No comments:
Post a Comment