Maduka 95 ya kubadilisha Fedha yasitisha Biashara - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Thursday, January 25

Maduka 95 ya kubadilisha Fedha yasitisha Biashara



MADUKA 95 kati ya 297 ya kubadilishia fedha yaliyokuwepo nchini kufikia katikati ya mwaka jana, yamesitisha biashara katika zoezi la uandikishwaji na utoaji upya wa leseni.

Kwa mujibu wa taarifa ya ufafanuzi kwa Nipashe iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uzimamizi wa Mabenki wa Benki Kuu (BoT), Kened Nyoni, maduka 64 hayakuomba leseni kama ilivyotakiwa kisheria Juni, mwaka jana.

Kwa mujibu wa ufafanuzi huo wa juzi, maduka 233 yaliwasilisha nyaraka muhimu kwa ajili ya maombi ya leseni na 64 yaliruhusiwa kuendelea na biashara, huku 31 yakiamua kufunga, na 138 BoT inafanya mapitio ya taarifa zake.

"Kati ya maduka 297 yaliyotakiwa kuomba upya leseni zao, maduka 64 hayakuwasilisha nyaraka yoyote... baada ya kupitia nyaraka za maduka 233, maduka 31 yaliamua kufunga biashara," alibainisha.

Taarifa ya BoT Juni, mwaka jana, ilionyesha kuwa maduka hayo yamepewa miezi mitatu kukamilisha usajili mpya kwa lengo la kuboresha usimamizi na kuweka mfumo wa kisasa utakaoleta tija katika mabadiliko ya uchumi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, BoT iliongeza mtaji wa maduka hayo kutoka Sh. milioni 100 hadi Sh. milioni 300 kwa yale ya daraja A.

Aidha, BoT ilipandisha mtaji kutoka Sh. milioni 250 hadi Sh. bilioni moja kwa maduka ya daraja B na kuongeza amana zisizo na faida kutoka dola za Marekani 50,000 hadi 100,000 (sawa na Sh. milioni 112 hadi Sh. milioni 224).

Aidha, Benki Kuu katika masharti yake kwa biashara hiyo ya kubadilisha fedha za kigeni ilizuia wenye hisa, wakurugenzi, mmoja wa mameneja au mfanyakazi kuwa kwenye duka zaidi ya moja.

Maduka yote yalitakiwa kufunga kamera maalum za ulinzi za CCTV, masharti hayo yalitaka, "ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zote muhimu za ulinzi na usalama kama zilivyoanishwa kwenye kanuni za mwaka 2015".

Aidha, wamiliki wa maduka hayo kwenye usajili wanatakiwa kutoa taarifa zao binafsi, ikiwamo chanzo cha mapato yaliyowezesha kuwepo kwa duka husika, na kueleza kwa undani kila kilichojazwa kwenye fomu mahali kilipo kwa kuwa kitafuatiliwa kwa kina.

Nyoni alisema Januari 2, mwaka huu, BoT ilitoa notisi kwa wafanyabiashara ambao hawajakamilisha nyaraka za usajili na walioshindwa kufikia vigezo vilivyotakiwa.

"Kwa kuzingatia kuwa maombi mengine yaliletwa dakika za mwisho (kelekea Desemba 31, mwaka jana), tumeongeza siku 30 kwa ajili ya mapitio kwa ambao hawakuwa wamekamilisha nyaraka za mwisho wafanye hivyo kuruhusu leseni kutolewa Januari 31, mwaka huu," alifafanua.

Alisema kwa kipindi cha kusubiri leseni maduka yaliyo kwenye utaratibu wa kupata leseni yanaruhusiwa kuendelea na kazi za kila siku.

MWAKA 1992Maduka ya kubadilishia fedha za kigeni yana historia fupi nchini kutokana na kuanzishwa na Sheria ya Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 ambayo inampa Gavana wa BoT mamlaka ya kuanzisha maduka ya kuuza na kununua fedha za kigeni na pia mamlaka ya kutunga kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya kusimamia maduka hayo.

Kanuni za kwanza zilitungwa na Gavana mwaka 1999, lakini kwa kuwa maduka hayo hayakuwa mengi hakukuwa na masharti magumu mpaka mabadiliko ya kanuni ya mwaka 2015 ambayo yalichangiwa pamoja na mengine, serikali kutambulisha mfumo mpya wa ukusanyaji kodi kwa kupitia mashine za kodi za kielektroniki (EFD).

Ndipo likaja tangazo la Juni 30, mwaka jana kwenye gazeti la serikali ambalo lilitata mchakato huo wa usajili upya kumalizika Septemba kabla ya kuongezwa muda mara mbili mpaka Januari 31, mwaka huu.

Habari zinadai masharti mapya ya Serikali yanatokana na BoT, kwa kushirikiana na vyombo vingine, kubaini maduka mengi yalikuwa yanaficha mitaji halisi.

Imeelezwa vitabu vya mahesabu vya maduka mengi vilionyesha mitaji ambayo siyo halisi, na baadhi kudai kupata hasara kila mwaka.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here