Simba kujichimbia tena Morogoro - MKWELITZ BLOG

Breaking

.

.

.

.

Friday, January 26

Simba kujichimbia tena Morogoro


KIKOSI cha Simba kinatarajia kwenda tena Morogoro au Zanzibar kwa ajili ya kuanza maandalizi ya kuwavaa wapinzani wao katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, klabu ya Gendarmarie Nationale kutoka Djibouti, imefahamika.

Vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba ambao wanadhaminiwa na Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya SportPesa wanatarajia kuwakaribisha Gendarmarie katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Februari 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah "Try Again" alisema jana kuwa uamuzi kamili utafanywa katika kikao cha pamoja na benchi la ufundi baada ya kumaliza mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Majimaji itakayofanyika Jumapili.

Salim alisema uongozi wa klabu hiyo unaamini kuwa kambi hiyo watakayokaa itasaidia kuwaweka wachezaji tayari kupambana kusaka matokeo mazuri katika mchezo wao wa kwanza wa kimataifa ambao utakuwa ni mtihani wa kwanza wa kimataifa kwa kocha mpya Mfaransa, Pierre Lechantre.

"Jumatatu wachezaji watapumzika lakini tutakuwa na kikao na benchi la ufundi kwa ajili ya kuamua kambi itakuwa wapi, kama ni Zanzibar au Morogoro, ila mazoezi wataanza Jumanne na baadaye ndiyo wataingia kambini," alisema kiongozi huyo.

Aliongeza kuwa mbali na kuandaa timu yao, vile vile wameunda "kikosi kazi" ambacho kazi yake maalumu kuwapeleleza wapinzani kabla hawajafika nchini na hatimaye kujipanga kuwakabili.

Baada ya wiki mbili, Simba itasafiri kuelekea Djibouti kuwafuata wenyeji wao ambao wanatumia uwanja wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 40,000.

Katika kuimarisha kikosi chake, Simba iliamua kuimarisha benchi lake la ufundi na vile vile kuboresha safu ya ulinzi kwa kumsajili beki wa kati kutoka Lipuli, Asante Kwasi, ambaye ni raia wa Ghana.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Responsive Ads Here