MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemtaka
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) anayekabiliwa na mashitaka
ya uchochezi, afike mahakamani leo kujieleza kwa nini asifutiwe dhamana.
Lissu anatakiwa ajieleze kwa sababu yeye a mdhamini wake
hawakufika mahakamani jana wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kutoa
uamuzi wa pingamizi la upande wa utetezi.
Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba alitoa amri hiyo jana baada
ya Wakili wa Serikali Mkuu, Mutalemwa Kishenyi kuomba Mahakama itoe hati ya
kumkamata Lissu kwa sababu ya kutokufika mahakamani.
Awali akitoa uamuzi huo, Hakimu Simba alitupilia mbali
pingamizi la upande wa utetezi na kuruhusu upande wa Jamhuri kuleta upya
mashitaka mawili ya uchochezi, ambayo hapo awali yalifutwa kwa kuwa hayakuwa na
kibali cha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Alisema awali mashitaka hayo yaliondolewa kwa sababu
hayakuwa na kibali lakini sasa ameyakubali kwa sababu yamewasilishwa pamoja na
kibali cha DPP, pia upande wa Jamhuri ulikuwa na haki ya kurekebisha mapungufu
na kuyaleta tena mashitaka hayo mahakamani.
Hata hivyo, baada ya kutolewa kwa uamuzi huo, Wakili wa
Utetezi, Peter Kibatala alidai hawajaridhika, hivyo wanatarajiwa kukata rufaa
kuupinga kwa sababu mashitaka hayo yalipofutwa yalikuwa yamekufa.
Aidha, aliiomba Mahakama kutoyasoma mashitaka hayo hadi
rufaa yao itakaposikilizwa katika Mahakama Kuu na kutolewa uamuzi. Wakili wa
Serikali Mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo
umekwishakamilika.
Hivi karibuni upande wa utetezi uliwasilisha pingamizi hilo,
baada Wakili Kishenyi kuomba kuwasomea washtakiwa hati iliyofanyiwa marekebisho
kwa kuongeza mashitaka mawili, ambayo awali yalishafutwa. Katika pingamizi
hilo, wakili alipinga washtakiwa hao kusomewa upya mashitaka hayo kwa kuwa
mashtaka mapya, hayatofautiani na yale yaliyofutwa mahakamani hapo Juni 28, mwaka
huu.
Akijibu hoja hizo, Kishenyi alidai shtaka la kwanza na la
tano ni kama hayakuwepo mahakamani na kwamba kuondolewa kwake sheria haikatazi
kuyarudisha tena.
Mbali na Lissu washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni
Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi wa gazeti hilo, Jabir Idrisa
na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.
Wanadaiwa kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, Dar es
Salaam, kwa lengo la kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar, Jabir, Mkina na
Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa za uchochezi zenye kichwa
cha habari kisemacho, ‘Machafuko yaja Zanzibar’.
Katika mashtaka yanayomkabili Mehboob, anadaiwa, Januari 13
katika jengo la Jamana, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa
na taarifa za uchochezi, pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati
ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.
SOURCE:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment