NDEGE mpya ya kwanza iliyonunuliwa na serikali kwa ajili ya
kutumiwa na Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), imetua kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam (JNIA), ikitokea nchini Canada
ilikotengenezwa.
Akizungumza baada ya kuwasili kwa ndege hiyo, Katibu Mkuu wa
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamriho alisema ndege ya
pili inatarajiwa kuwasili baada ya wiki moja.
“Baada ya kuwasili ndege ya pili ndipo yatafanyika mapokezi
rasmi, yatakayoongozwa na Rais Magufuli kwa tarehe itakayotangazwa baadaye,”
alisema Chamriho.
Taarifa ya awali iliyotolewa na ATCL mwishoni mwa wiki,
ilieleza kuwa ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 76 ikiwa na marubani
wanne kutoka Canada, ilianza safari ya kuja nchini tangu wiki mbili zilizopita
ikipitia miji ya ReykjavÃk, Southampton, Malta, Luxor na Addis Ababa Ethiopia.
Ilieleza kuwa ndege hizo, zitaanza kufanya safari zake mara tu baada ya
kukamilisha mchakato wa kusajiliwa na Mamlaka ya Usalama wa Anga Tanzania
(TCAA).
“Kwa kuwa zitakuja zikiwa na usajili wa nchini Canada,
tutalazimika kutumia siku mbili hadi tatu kuziingiza kwenye usajili wa TCAA
pamoja na kukamilisha taratibu nyingine za kisheria ili ziweze kupata ruhusa ya
kufanya safari za hapa kwetu,” ilieleza.
Iliongeza kuwa safari ya kwanza ya ndege hiyo, inatarajiwa
kufanyika Septemba 27, mwaka huu kwenda jijini Mwanza.
“Tutakuwa na madaraja mawili yaani daraja la uchumi (Economy
Class) litakalohusisha abiria 70 na daraja la biashara (Business Class)
litakalohusisha abiria sita kwa kila ndege,’’ ilibainisha. Ilitaja baadhi ya
maeneo ambayo shirika hilo litaboresha zaidi safari zake kuwa ni Dodoma,
Mwanza, Arusha, Mbeya, Kigoma, Tabora, Mpanda, Kilimanjaro, Mtwara, Zanzibar,
Pemba, Bukoba na Visiwa vya Comoro. Ujio wa ndege hizo unatajwa kuwa utaleta
mapinduzi makubwa kihuduma na kiutendaji kwa shirika hilo.
Tayari kampuni hiyo imebainisha kwamba imeunda kikosi kazi,
kinachosimamia masuala mbalimbali likiwemo suala la mafunzo ya watendaji wake
mbalimbali ili kuendana na matakwa ya biashara hiyo kwa sasa likiwemo suala la
kufanya biashara kwa ushindani. Ujio wa ndege hizo ni ahadi ya Rais John
Magufuli aliyoitoa mara baada ya kuingia madarakani, ambapo kupitia bajeti ya
wizara hiyo ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ilitenga pia kiasi cha fedha
kwa ajili ya ununuzi huo.
Kwa mujibu wa Waziri wake, Profesa Makame Mbarawa wakati
akisoma makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka 2016/17, serikali imejipanga
kukamilisha ununuzi wa ndege mbili aina ya Bombardier Q400 kwa ajili ya ATCL
ili kufufua safari za ndani za kampuni hiyo.
Hadi sasa ATCL ina ndege moja aina ya Bombadier Q300, hivyo
ujio wa ndege hizo utaifanya kuwa na ndege nne zinazotoa huduma ya usafiri wa
anga nchini.
SOURCE:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment