KUTOKANA na
kauli ya Rais John Magufuli kuwa
anafahamu wapo wananchi wameficha fedha nyumbani,na wanazuia mzunguko wz fedha
wachumi wametoa maoni yao na kusema hao ni wahujumu uchumi na wanapaswa
kutafutwa na vyombo vya dola na washtakiwe.
Akitoa maoni
yake jana jijini Dar Salaam, Mhadhiri Mwandamizi wa Masuala ya Uchumi wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana alisema uhai wa uchumi ni uwepo
wa mzunguko wa fedha za kutosha.
Dk Bana
alisema uchumi wa taifa lolote ni lazima katika kazi na shughuli za kimaendeleo
na kijamii fedha ziwepo ili kufanya mzunguko uongezeke na kukuza uchumi, lakini
uchumi huathirika iwapo kutatokea watu wanauhujumu kwa njia mbalimbali.
“Baadhi ya
watu wanaamua kuficha fedha na hiyo inaathiri mtiririko wa fedha na wanaleta
mfumuko wa bei, hawa sasa wanafanya hila kuzorotesha uchumi,” alisema Dk Bana
na kuongeza kuwa kama fedha ni halali, kwa nini mtu afiche na kusema kuwa benki
ndio mahali pekee salama kwa kutunza fedha na kama wapo watu wanatoa fedha
benki na kuzificha majumbani wana hila za kuhujumu uchumi.
Alifafanua
kuwa katika uhai wa taifa lolote kukiwa na mzunguko wa fedha wa kutosha katika
jamii, husaidia kuimarisha thamani ya fedha na kwamba kama mzunguko huo
utaathiriwa kwa makusudi unaweza sababisha hali mbaya ya uchumi.
Hata hivyo,
alisisitiza kuwa jambo la msingi la kufanya sio kuchapisha fedha mpya, bali ni
kuhakikisha serikali inawabana wala rushwa na mafisadi ambao ndio wanachangia
uchumi kuyumba.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania, Johnson Minja alisema
wanaoficha fedha kwa makusudi ni wahujumu uchumi na wanapaswa kusakwa na
kuchukuliwa hatua.
Minja
alisema fedha sio mali ya mtu binafsi ni mali ya serikali na inapaswa kutumika
kwa makusudi stahiki ambayo ni pamoja na kumwezesha mwananchi kufanya malipo
mbalimbali na ndio maana fedha zote zina namba na saini ya waziri husika pamoja
na gavana wa Benki Kuu.
“Watu
waelewe kuwa fedha sio mali yao hata kama unazimiliki ni mali ya serikali na
hupaswi kuzificha, ni lazima ziingie kwenye mzunguko wa fedha unapoficha ni
kosa la kuhujumu uchumi na unapaswa kuchukuliwa hatua,” alisema Minja.
Alisema watu
wanaoficha fedha nyumbani wengi wao ni wahalifu na wanafanya hivyo kwa sababu
wanafahamu fedha hizo wamezipata isivyo halali na ni vyema vyombo vya uchunguzi
nchini vikawamulika na kuwashughulikia kwa sababu wanahujumu uchumi kwa maslahi
binafsi.
Hata hivyo, alisema
pamoja ya kuwepo na tatizo hilo la baadhi ya watu kuficha fedha kwa makusudi,
wapo pia wananchi walioficha fedha zao kwa sababu ya uelewa mdogo wa masuala ya
fedha.
Alisema hivi
sasa nchini kuna tatizo la kusuasua kwa mzunguko wa fedha unaosababishwa na
kupanda kwa bei za kodi mbalimbali hivyo wananchi wana hofu ya kuagiza bidhaa
nje kwa kuwa watashindwa kuuza kutokana na bei kuwa kubwa.
Alishauri
serikali kuangalia jinsi ya kurudisha uchumi katika hali ya kawaida ili
biashara zifanyike na watu waagize bidhaa nje.
No comments:
Post a Comment