Baadhi ya hao ni Mameneja wa Man City Pep Guardiola na Mchezaji
wake Yaya Toure aliempiga marufuku kucheza na ghafla Jana kumchezesha na
Staa huyo kupiga Bao zote 2 na kuwapa ushindi City wa 2-1 dhidi ya
Crystal Palace.
Pia Jose Mourinho, Meneja wa Man United ambae Jana walipokwa
ushindi baada Arsenal kusawazisha Dakika ya 89 na kupata Sare 1-1 lakini
hilo limeendeleza Rekodi ya Mourinho kutofungwa na Arsene Wenger katika
Mechi 15 za EPL ambazo ameshinda 8 na Sare 7.
Vile vile, Nahodha wa Man United Wayne Rooney ambae pia ni Nahodha
wa Timu ya Taifa ya England aliongea kuhusu kusakamwa sana kwake.
NINI WAMESEMA?
-WAYNE ROONEY:
Wayne Rooney amedai amekuwa akisakamwa mno wakati akiichezea England na hilo ni tendo la fedheha kubwa.
Rooney ameichezea England Mechi 119 akiwa ni wa pili katika
Historia kwa kucheza Mechi nyingi nyuma ya Kipa Peter Shilton aliecheza
Mechi 125 na pia ndie Mfungaji Bora katika Historia ya Nchi hiyo.
Hivi karibuni Jarida moja huko England lilitoa Picha za Rooney
akinywa Pombe Hotelini waliyokuwa wakikaa Timu ya England ingawa Siku
hiyo Kikosi chote kilikuwa kimepewa Ofu na Meneja Gareth Southgate.
Akiongea hapo Jana mara baada ya Mechi ya Man United na Arsenal, Rooney aliwashambulia wanaomsakama na kudai wanakosa heshima.
Alisema: "Inaonyesha kama Wanahabari wanaandika Wasifu wa Kifo
changu na hilo sitaruhusu litokee. Yanayotokea ni fedheha. Napenda
kuchezea Nchi yangu na naskia fahari mafanikio yangu. Bado sijaisha!"
Nao Wachezaji wa zamani wa England, Ian Wright na Alan Shearer, wamejitokeza kumpa sapoti Rooney.
Akiongea hapo Jana, Ian Wright, alisema: "Kwa Miaka Mitatu au Minne
wamekuwa wakimshambulia. Nimefurahi mno sasa anajibu mapigo. Pigana
Wayne!"
Nae Nahodha wa zamani wa England Alan Sherer amesema: "Siku zote
amejitolea kwa nguvu zote kuichezea England. Kama alipewa Ofu na kuamua
kubaki Hotelini na kupata kinywaji hakufanya kosa labda ingekuwa ameenda
kinyume na Meneja!"
-YAYA TOURE:
Mara baada ya Jana kuchezeshwa kwa mara ya kwanza baada Miezi
Mitatu baada kupigwa stopu na Meneja Pep Guardiola kufuatia ugomvi na
Wakala wake, Yaya Toure ambae alifunga Bao zote 2 wakati Man City
inaifunga Crystal Palace 2-1 amefunguka na kusema hakushangazwa kuitwa
kuichezea tena Timu hiyo.
Toure, mwenye Miaka 33, ameeleza: "Nilikuwa tayari kiakili na nilijua ipo Siku Meneja ataniita!"
Toure, ambae ameiwezesha City kutwaa Ubingwa EPL mara 2, Jana
alipokewa vizuri na Mashabiki wa Timu hiyo waliokuwa wakimuimba Mechi
nzima.
Mwishoni mwa Mechi hiyo na Palace Wachezaji wote wa City walimshangilia Toure na kumsindikiza kwa Makofi hadi nje ya Uwanja.
-JOSE MOURINHO:
Kwa mujibu wa Meneja wa Man United Jose Mourinho Timu yao ndio Timu
ambayo haina bahati baada ya Jana Arsenal kusawazisha Dakika ya 89 na
kupata Sare ya 1-1.
Mourinho ameeleza: "Sina la kusema kuhusu Wachezaji wangu lakini
nawaonea ruhuma kwani hiyo ni kama tumefungwa wakati Arsenal wanaona
wameshinda!"
Aliongeza: "Sare hizi na Burnley, Stoke na Arsenal ni kupoteza
Pointi 9. Tungepata Pointi 6 tu tuko 4 Bora na karibu ya kileleni!
Tunajua hivi sasa sie ndio Timu isiyo na bahati kwenye EPL!"
Man United wameshapambana na Manchester City, Liverpool, Chelsea na
Arsenal bila ushindi wakitoka Sare 3 na kufungwa na Chelsea tu.
Hivi sasa wapo Nafasi ya 6 wakiwa Pointi 5 nyuma ya Arsenal ambao
wako Nafasi ya 4 na ambao wapo Pointi 2 nyuma ya Vinara Liverpool.
source:soka in bongo
No comments:
Post a Comment