OCPD wa Bomet, Bw Samson Rukunga alisema Pasta John Kipsiele Makibior alipatikana akiwa amekufa na mwili wake kuharibiwa katika kile kinachoonekana kuwa mauaji ya kinyama.
Alisema polisi walifika mahali hapo na kuchukua mwili uliokuwa umetupwa karibu na kijito, nyumbani kwake Kakimirai, Bomet Mashariki.
Aliongeza kuwa kifaa kilichotumika kwa mauaji ya pasta huyo pia kilipatikana mahali hapo.
Alieleza kuwa pasta huyo anashukiwa kuuawa na mlishaji wake wa mifugo ambaye alitoweka baada ya tukio hilo.
“Polisi wameanzisha msako wa mshukiwa aliyetoroka,” alisema.
Bw Rukunga alisema mwili wa marehemu ulikuwa umekatwa kichwani, shingoni na vidole kukatwa kabisa.
Alieleza kuwa uchunguzi wao wa mapema umeonyesha kuwa marehemu alikuwa ametofautiana na mfanyakazi wake.
Pia aliomba umma wenye habari kuhusu mshukiwa kupiga ripoti kwa polisi.
Mwili wa marehemu ulipelekwa kuhifadhiwa katika mochari ya hospitali ya Tenwek.Marehemu alifahamika kwa kuonyesha filami za injili katika kaunti za Kericho na Bomet kama njia yake ya kueneza injili.
Viongozi wa kidini katika eneo hilo, ambao ni pamoja na askofu Robert Langat wa AGC Kenya,walieleza kushtuliwa na mauaji hayo na kuwataka polisi kuharakisha uchunguzi wao na kumkamata mshukiwa.
No comments:
Post a Comment